Dar es Salaam
Vodacom Tanzania Plc. kampuni inayoongoza ya huduma za teknolojia na mawasiliano leo imeungana na wadau wengine kuadhimisha kilele cha Wiki ya Maji ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani, ambayo mwaka huu ina kauli mbiu: “Maji Chini ya Ardhi, Hazina isiyoonekana kwa Maendeleo Endelevu”.
Akiongea wakati wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa M-Pesa, Vodacom Tanzania, Epimack Mbeteni alisema, “Kama sote tunavyofahamu, Serikali yetu imeweka dhumuni la kuhakikisha Tanzania inakuwa ya kidijitali hasa kwenye malipo ya Ankara mbalimbali zikiwamo za Serikali. Hili linaendana na dhima ya kampuni yetu ya kuhakikisha tunaiwezesha jamii yetu kuishi kidijitali, watu waweze kuwasiliana kidijitali, waweze kufanya malipo kidijitali, waweze kutoa huduma mbalimbali kidijitali. Vodacom inaamini kupitia huduma ya M-Pesa, Mwananchi atafanya malipo, na malipo hayo yatawezesha upatikanaji wa maji kwa huduma endelevu. Kupitia huduma za M-Pesa mteja wetu anaweza kulipia huduma mbalimbali za Serikali”.
M-Pesa inawezesha watumiaji zaidi ya milioni 1.6 nchini kulipa Ankara zao za maji kidijitali kwenda kwa taasisi 23 za maji katika mikoa yote nchini. Malipo haya ya huduma za maji yanayopitia M-Pesa yanafika kiasi cha Shilingi bilioni 36 kwa mwaka. Huduma hii inaokoa muda kwa mtumiaji na vilevile kuzipa taasisi husika nafasi ya kufanya shughuli zingine. Kwa njia hii Vodacom Tanzania inasaidia taifa kutimiza lengo endelevu (SDG) namba sita ambalo linaitaka serikali kuhakikisha upatikanaji wa huduma za maji safi na maji taka.
“Tunataka kuona wateja wetu na watanzania kwa ujumla wakiokoa muda, hakuna sababu ya wao kupanga foleni kulipia Ankara za maji ilhali anaweza kulipia kupitia simu yake ya mkononi, M-Pesa tupo hapa kuboresha maisha ya Watanzania wote,” aliongeza Mbeteni.
Lengo kuu la maadhimisho haya hapa nchini ni kuungana na Mataifa mengine Duniani katika kutathmini utekelezaji, mafanikio, changamoto na kuainisha mikakati ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira pamoja na kusimamia utunzaji wa rasilimali za maji nchini.
Vodacom Tanzania Plc kupitia asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Vodacom Tanzania Foundation, imekuwa ikijihusisha na maswala ya utunzaji mazingira na usimamizi na upatikanaji wa maji safi kwa miaka kadhaa. Kampuni hii ya teknolojia imekuwa mstari wa mbele kusaidiana na serikali kuu kutimiza lengo endelevu namba 13 (SDG 13) linalolenga kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa. Kwa mfano, Vodacom imejihusisha katika mradi wa “Kijanisha Dodoma” kwa kuchangia zaidi ya Shilingi milioni 300 na kupanda miti zaidi ya 96,000 katika maeneo mbalimbali jijini Dodoma. Pamoja na mradi huo, Vodacom Tanzania, kupitia asasi ya Vodacom Tanzania Foundation, pia imekuwa na miradi kadhaa ya utunzaji mazingira katika mikoa mingine nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...