Na. WAF - Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuwekeza kwenye afya ya uzazi,mama na mtoto ili kuwa na jamii yenye afya na ustawi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiongea kwenye kipindi cha Good Morning kinachorushwa na Wasafi FM ikiwa ni sehemu ya vipindi maalum kuelekea siku ya wanawake duniani.

Waziri Ummy amesema kuwa ili kuwa na uzazi salama Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu itaendelea kuweka fedha  katika eneo hili katika bajeti zake kila mwaka ikiwemo huduma kwa wajawazito, huduma za uzazi wa dharura na huduma kwa watoto wachanga.

Hata hivyo Waziri Ummy ametoa tahadhari juu ya matumizi holela ya vidonge vya dharura vya kuzuia mimba (P2) kwamba matumizi holela na ya mara kwa mara ya P2 yana madhara kwa Afya ya mwanamke kwa kumuweka katika hatari ya kupata Ugumba na Saratani.

"Vidonge hivi vya P2 sio vya kunywa kila siku, tutaendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi ili jamii iweze kuelewa pia tutaendelea kuweka fedha kwenye masuala ya Afya ya uzazi, mama na mtoto". Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri ametoa wito kwa wazazi na walezi kutoa elimu kwa watoto wao juu ya afya na mabadiliko ya mwili ikiwemo vichocheo vya hisia bila kuona aibu.

Pia amesema Wasichana wa sasa hasa wa vyuoni wanaogopa kupata mimba kuliko kupata Ukimwi jambo ambalo ni hatari kwa afya zao kwani wanajiweka katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukizwa.

"Usipomueleza mtoto vizuri masuala ya Afya yake, mwili wake ataenda kuyapata kwenye njia ambazo sio sawa kama kwenye mitandao ya kijamii na kwa marafiki wanaozunguka jambo ambalo linamuweka kwenye hatari ya kupata maambukizi". Amesema Mhe. Ummy.

Waziri Ummy amesema ili kutumia vizuri njia za uzazi wa mpango za Kisasa unatakiwa kwenda kwa daktari kujua hali na kupata ushauri na kuendelea kusisitiza matumizi ya njia za asili kama kuangalia kalenda ambayo kwa sasa unaweza kutumia hata simu janja ya mkononi (Smartphone).

Vile vile Waziri Ummy ametoa wito kwa wanawake kuwa na tabia ya kuchunguza afya zao mara kwa mara ili kuepuka magonjwa kama Saratani ya Kizazi na Saratani ya Matiti kwani hivi sasa kati ya wanawake 100 wanaofanyiwa uchunguzi wanawake 40 hupatikana na saratani ya mlango wa kizazi.

Ameitaka  jamii kuzingatia mfumo bora wa maisha na kuacha matumizi ya chumvi nyingi, sukari na mafuta mengi  wakati wa kuandaa chakula.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...