Serikali yaidhinisha shilingi bilioni 300 za kitanzania kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi na Miundombinu ya awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza leo Mtumba jijini Dodoma, wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Balozi Pindi Chana alisema kuwa, Ofisi yake imeendelea kuratibu utekelezaji wa maamuzi ya Serikali ya kuhamia Dodoma kwa lengo la kufanya Serikali kuwa katikati ya nchi na kuwa karibu na Mikoa yote nchini ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kufanikisha hilo tayari Serikali imeidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi huo.
“Katika mwaka wa fedha 2021/22 jumla ya shilingi bilioni 300 ziliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara zenye urefu wa kilomita 51.2 zinazojengwa kwa kiwango cha lami” alisema Balozi Chana
Aidha, aliongeza kuwa tayari uzinduzi wa ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wizara na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mji wa huo ulishafanyika Desemba mwaka 2021. Hivyo, ujenzi wa ofisi hizo unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwaka 2022/2023 ambapo zitakapokamilika zitatosheleza mahitaji ya wafanyakazi wa Wizara zote.
Katika hatua nyingine, Balozi Chana alisema kuwa Serikali imeendelea kuhakikisha inadhibiti matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya kwa lengo la kuwanusuru wananchi wake kuathirika na dawa hizo.
Ambapo, katika kipindi hiki, Serikali imefanikiwa katika udhibiti wa dawa ambapo jumla ya kilo 35,227.5 zilikamatwa zilizojumuisha kilo 1124.52 za Heroin, gramu 811.3 za Cocaine, kilo 22,741.10 za Bangi, kilo 10,931.72 za Mirungi, gramu 4.92 za Morphine, na kilo 428.60 za Methamphetamine.
Balozi Chana, alifafanua “Kati ya dawa za kulevya zilizokamatwa, kilo 859.36 zilikamatwa siku moja kwa watuhumiwa saba raia wa Iran na kuvunja rekodi kuwa ni ukamataji wa kwanza wa kilo nyingi zilizokamatwa kwa pamoja tangu nchi yetu ipate uhuru”.
Vilevile, ekari 185 za mashamba ya Bangi na ekari 10 za Mirungi ziliteketezwa mkoani Pwani katika Wilaya ya Rufiji.
Mbali na hayo, jitihada zingine zinazofaywa na Serikali ni pamoja na kutoa huduma ya matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya ambapo kliniki sita za tiba ya Methadone zimeanzishwa katika maeneo ya Songwe katika mji wa Tunduma, Jijini Arusha na Kliniki zingine nne zipo Jijini Dar es Salaam katika maeneo ya Tegeta, Segerea, Mbagala na Kigamboni.
Uanzishwaji wa kliniki hizo kunafanya jumla ya kliniki 15 kuwepo nchini zikihudumia zaidi ya waathirika 10,600 wa dawa za Kulevya kila siku. Vilevile, Serikali imekuwa ikisimamia upatikanaji wa uhakika wa dawa ya Methadone kwa ajili ya tiba ya waraibu wa Heroin kwa kusimamia uagizaji, usambazaji na udhibiti wake.
Balozi Chana anaongeza “vilevile, vijana 200 wanaopatiwa matibabu kwenye kliniki za Methadone wamejumuishwa katika Programu ya Kukuza Ujuzi kupitia Vyuo vya VETA ili kuwajengea ujuzi wa kufanya kazi za kiuchumi na kuachana na dawa za kulevya”
Sambamba na hilo na vimeanzishwa vilabu vya kupinga dawa za kulevya mashuleni na elimu imetolewa kwa walimu 66 ili kuwawezesha kusimamia klabu hizo. Aidha, Elimu juu ya tatizo la matumizi na biashara ya dawa za kulevya iliwafikia wanachuo 1,700 katika vyuo mbalimbali nchini.
Vilevile, elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya imekuwa ikitolewa kupitia vyombo vya habari kama vile televisheni, magazeti, warsha za Kitaifa, Mbio za Mwenge, makongamano pamoja na mitandao ya kijamii kuhusu madhara ya dawa hizo ambapo inakadiliwa zaidi ya wananchi millioni 10 wamefikiwa na elimu hiyo. Ambapo jitihada hizo zimetajwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia wimbi la vijana kuingia kwenye matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...