Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali imeendelea kuimarisha Huduma na Mafunzo kwa Watu wenye Ulemavu nchini ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu iliyokuwa imechakaa katika Vyuo vya Watu Wenye Ulemavu.
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita madarakani, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alisema kuwa Serikali imekarabati mabweni katika Chuo cha Yombo – Dar es Salaam hivyo kuongeza udahili kutoka wanafunzi wenye Ulemavu 64 hadi 120, Chuo cha Masiwani, Jijini Tanga ambacho kimekarabatiwa miundombinu yake ikiwemo mabweni, nyumba za walimu, madarasa, Ofisi na uzio ambapo Chuo hicho kitafunguliwa mwishoni mwa mwezi Machi, 2022 na kitadahili wanafunzi wenye ulemavu 96.
Waziri Ndalichako alitaja Chuo kingine kichokarabatiwa kuwa ni Chuo cha Luanzari, Tabora ambacho kilifungwa tangu mwaka 1997 kilifunguliwa tarehe 01 Agosti, 2021 ambapo kwa sasa kina wanafunzi 48 wenye ulemavu.
“Tumepokea shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya kuendelea na ukarabati wa vyuo vitano vya Watu wenye Ulemavu nchini na taratibu za manunuzi zimekamilika. Aidha Serikali imepanga kujenga vyuo vipya viwili na kuendelea na ukarabati wa vyuo vitano vya Watu wenye Ulemavu” Alisisitiza Waziri Ndalichako.
Aidha, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu ikiwemo miundombinu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja, kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI yamejengwa mabweni 50 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi wenye ulemavu 4,000 wa shule za msingi kwa gharama ya shilingi bilioni 4.
Waziri Ndalichako aliongeza “Ujenzi wa vyumba vya madarasa 12,000 ya Sekondari na Madarasa 3,000 katika vituo shikizi vya shule za msingi, ujenzi wa shule mpya 235 za kata na ujenzi wa shule 10 maalum za sekondari za wasichana umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza fursa za elimu kwa watu wenye ulemavu kwani shule zinapokuwa mbali na maeneo wanayoishi inakuwa vigumu zaidi kwao kupata elimu”
Alifafanua kuwa hatua ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuboresha huduma kwa jamii kama maji, barabara, ujenzi wa vituo vya afya 233, imekuwa faraja kubwa kwa watu wenye ulemavu kwani walikuwa ni waathirika zaidi na kukosekana kwa huduma hizo katika maeneo yao.
Serikali imeendelea kuwawezesha Watu wenye Ulemavu kiuchumi kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020. Katika mwaka wa fedha 2021/22 jumla ya shilingi bilioni 68.19 zimetengwa kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa ajili ya vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu. Katika fedha hizo jumla ya shilingi bilioni 1.94 zimetolewa kwa ajili ya vikundi 382 vya Watu wenye Ulemavu.
Vilevile, kupitia fedha za UVIKO -19 jumla ya shilingi bilioni 5 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha biashara kwa Machinga, Ofisi ya Rais – TAMISEMI inaratibu utekelezaji wake ambapo watu wenye ulemavu pia watanufaika na hatua hiyo ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...