*Ni matunda ya usimamizi imara wa Ofisi ya Msajili Hazina

*Mengi makubwa yafanyika mwaka mmoja wa Rais Samia

 

Na Mwandishi Maalumu, Dodoma


OFISI ya Msajili wa Hazina imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 539.39 kutokana na mapato yasiyo ya kodi kati ya Machi 2021 na Februari 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 105 kutoka kiasi cha Sh bilioni 262.99 kilichokuwa kimekusanywa katika kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita.

Kauli hiyo imetolewa na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto jijini Dodoma alipokuwa akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha mwaka mmoja chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Makusanyo hayo ambayo ni moja ya majukumu ya Msajili wa Hazina, yamepata ufanisi kutokana na mapato kuimarika mwaka hadi mwaka hivyo kuongeza mapato yasiyo ya kodi yanayojumuisha Gawio, Michango ya 15% ya Mapato ghafi na mapato mengineyo.

Ufanisi huo uliotangazwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina inayosimamia Taasisi na Mashirika ya Umma 287, ikijumuisha kampuni na Taasisi 40 zinazomilikiwa na Serikali kwa hisa chache na Taasisi 10 za nje ya nchi, umetokana na usimamizi madhubuti wa serikali na maelekezo thabiti kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Ilivyookoa fedha za Umma

Aidha, sambamba ni hilo katika kuwajibika kwake na ikiwa ni utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria, Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imefanikiwa kuokoa Fedha za Umma na Mali za Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) zilizowekwa dhamana katika Benki ya Exim Tanzania.

Awali, kampuni hiyo ilishindwa kulipa deni la Dola za Marekani milioni 6.7, na baada ya majadiliano, Serikali ililipa Dola za Marekani milioni 2.7, hivyo kuokoa kiasi cha Dola Milioni 4 pamoja na mali za TFC kama maghala na jengo la ofisi vilivyokuwa zimewekwa dhamana.

Pia imewezesha Benki ya Maendeleo (TIB DFI) kurejeshewa fedha za Madeni ya Mikopo iliyokuwa hailipiki iliyotolewa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Kwa mujibu wa Msajili huyo, deni la TPDC lilikamilishwa Novemba 2021 ambapo kiasi cha Dola za Marekani milioni 34.39 zimelipwa huku deni la NHC – Mpaka kufikia 31 Desemba 31, 2021, NHC ilisharejesha kiasi cha Sh bilioni 30.16 na deni limebaki kiasi cha Sh 17.62 ambapo malipo yanaendelea kufanyika. Aidha deni la TANESCO – Mpaka kufikia Desemba 31, 2021, TANESCO ilisharejesha kiasi cha Shilingi bilioni 29.40 na deni limebaki kiasi cha Sh bilioni 15.58 na linaendelea kulipwa.

“Malipo ya madeni ya mikopo hii yameiwezesha Benki ya TIB DFI kuimarisha hali yake ya Ukwasi na kuwezesha utekelezaji wa majukumu yake,” alisema Msajili wa Hazina.


Upanuzi mkubwa Kilombero

Akizungumzia upanuzi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero, alisema Serikali kupitia Msajili wa Hazina pamoja na wanahisa wenza (Illovo Group) wameingia makubaliano kutekeleza mradi mkubwa wa upanuzi wa kiwanda kwa gharama ya kiasi cha Sh bilioni 571.6 (Dola za marekani milioni 238.5).

Uwekezaji huo unatarajiwa kuzalisha sukari tani 144,000 ambayo itaongeza uwezo wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kuzalisha sukari hadi kufikia tani 271,000 kutoka tani 127,000 za sasa.

Yaokoa shamba la bil. 152

Msajili pia ameokoa shamba la Mngeta - Kilombero Plantation Limited (KPL) kwa kulinunua kwa Dola za Marekani milioni 7.40. Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya Mthamini Mkuu wa Serikali, shamba la Mngeta lina thamani ya shilingi bilioni 152.19.

 

“Ni dhahiri kuwa uwekezaji huu ni mkubwa na Serikali itapata rudisho thabiti na endelevu” alisema Msajili na kuongeza kuwa Serikali iliamua kukabidhi mali hizi kwa Kampuni ya SUMA JKT ambayo inajishughulisha na vitega uchumi mbalimbali ikiwemo Kilimo cha Biashara, ambapo tayari shughuli za kilimo zimeanza.

 

NBC, Airtel mapato juu

 

Akizungumza utendaji wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache alisema taasisi yake imefanya majadiliano na wabia wenza na kusimamia kwa karibu matumizi yasiyo ya lazima na hivyo kushuhudia ongezeko la gawio kwa wanahisa. Alisema, mafanikio ya jitihada hizo yamejidhihirisha katika utendaji wa benki ya NBC ambayo imeongeza faida kabla ya kodi kutoka Sh bilioni 7 mwaka 2020 hadi Sh bilioni 60 mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 757.

Aidha alisema mapato kutoka Kampuni ya Airtel yameongezeka kutoka kiasi cha Sh bilioni 34.66 mwaka 2020/21 hadi kiasi cha Sh bilioni 70.22 katika kipindi cha miezi 8 ya mwaka 2021/22. Mapato haya yanajumuisha ulipaji wa gawio, mauzo ya minara na utekelezaji wa makubaliano maalumu ya wanahisa.

Akizungumzia ujenzi wa mfumo wa bajeti kwa Mashirika na Taasisi za Umma (PLANREP) alisema katika kuendelea kudhibiti matumizi ya Mashirika ya Umma, Ofisi imeanzisha Mfumo wa Mipango na Bajeti (PLANREP).

Alisema kumekuwepo na mafanikio makubwa kwa kuwekwa kwa mfumo huo kwa Taasisi, Wakala za Serikali na Mashirika ya Umma ambapo Taasisi zote zimefanikiwa kuingiza Taarifa zao za bajeti kwa ajili ya uchambuzi, idhini na kuanza kufanya matumizi kuanzia mwezi Julai 2021.

“Ofisi ya Msajili wa Hazina imefanikiwa kuchambua bajeti za Taasisi na Mashirika kwa mwaka wa fedha 2021/22 na inaendelea kusimamia bajeti za Taasisi hizo kupitia Mfumo huo ambao umeunganishwa na Mfumo wa Malipo Serikalini (MUSE),” alisema Mgonya.

Msajili huyo alisema kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina kama msimamizi mkuu wa uwekezaji wa Serikali kwa niaba ya Rais itaendelea kusimamia kwa karibu utendaji wa Mashirika na Taasisi za Umma ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata faida ya uwekezaji wake sambamba na kuongezeka kwa mapato yasiyo ya kodi ili kusaidia miradi ya maendeleo kwa faida ya Taifa na wananchi wote kwa ujumla

Msajili wa Hazina, Benedicto Mgonya akielezea mafanikio ya Ofisi yake katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita  chini ya uongozi wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Machi 18, 2022 jijini Dodoma.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...