Na. John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Duniani limetoa fursa muhimu ya kuwakutanisha wataalamu wa Kiswahili na watangazaji kwa Kiswahili, kujadili maendeleo ya lugha yao na kuweka mikakati ya kuzikabili changamoto zinazojitokeza ili Kiswahili kipige hatua zaidi na kuwawezesha kimapato watumiaji wake na taifa kwa ujumla.


Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Machi 18, 2022 jijini Arusha wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi wa kongamano hilo, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar kufunga Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili duniani.

Aidha, amesema Wizara zenye dhamana ya kusimamia utamaduni kwa Tanzania bara na visiwani zitaendelea kushirikiana kuhamasisha watangazaji wa Idhaa za Kiswahili na maofisa habari wote kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

“Wizara zetu zote mbili zinaamini kuwa Kongamano hili limetoa fursa kwa watangazaji wa idhaa za nchini kujifunza kutoka kwa watangazaji wa idhaa zilizoko nje ya nchi na vivyo hivyo kwa upande mwingine. Hivyo, nakuahidi kuwa tutaweka usawa hasa katika mambo ambayo yanahitaji maamuzi ya pamoja ama mashirikisho kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Amesisitiza Mhe Mchengerwa Pia amesema kuwawepo kwa Rais Mwinyi katika tukio hili ni ishara kwamba Serikali zote mbili siyo tu kwamba ziko bega kwa bega na wadau wa Kiswahili bali pia, zina dhamira ya dhati ya kuona kuwa Kiswahili kinapiga hatua zaidi kitaifa na kimataifa.

Amesema Wizara zitayaelekeza mabaraza ya BAKITA na BAKIZA kuyafanyia kazi maazimio yote yatakayojadiliwa katika Kongamano hili na kupeleka taarifa za ushughulikiaji wa maazimio hayo kwa idhaa zote.

Kongamano hilo limekuja na maazimio kumi na sita ambayo wameomba yatekelezwe ili kendelea kukikuza Kiswahili.

Amefafanua kuwa lugha yoyote hukua zaidi kwa kupewa majukumu, na amesema kwa sasa lugha Kiswahili imepewa majukumu mengi ya kuhudumia katika mikutano mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa na kwamba ni jukumu la wadau wa lugha hii kufanya jitihada kubwa ili kuhakikisha kwamba lugha hii inaendelea kutekelezwa ipasavyo.

Ametumia muda huo kuiomba Serikali kuwepo kwa vituo vya utamaduni kwenye balozi za Tanzania nje ya nchi ili kuendelea kukikuza Kiswahili kimataifa.

Pia amesema mafanikio ya Kiswahili yalikuwa ni maono ya Muasisi wa Taifa, Rais wa Awamu ya Kwanza wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mwl. J.K. Nyerere.

Katika tukio hili Mhe. Rais Mwinyi alizindua mfumo wa kufundisha Kiswahili na kutoa vyeti vya ushiriki na utambuzi kwa wadhamini na washiriki wa Kongamano ambapo yeye pia alikabidhiwa tuzo na Mhe. Mchengerwa kwa kutambua mchango wake wa kukuza Kiswahili.

Kongamano hili limehudhuriwa na washiriki takribani 200 wa redio na televisheni zinazotangaza kwa Kiswahili ndani na nje ya nchi, maofisa habari na wataalamu wa lugha ya Kiswahili na limebeba kaulimbiu “Tasnia ya Habari kwa Maendeleo ya Kiswahili Duniani”.

Pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliongozwa na Mhe. Mchengerwa na Naibu wake Mhe. Pauline Gekul, pia Katibu Mkuu. Dkt, Hassan Abbasi ambaye awali leo alitoa mada na Naibu wake Saidi Yakubu ambaye anasimamia eneo la lugha ya Kiswahili katika Wizara hiyo.





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...