Shirikisho la mchezo wa kuogelea duniani (FINA) limeahidi kusaidia Chama Cha mchezo wa kuogelea nchini (TSA) kutatua changamoto mbalimbali ikiwa bwawa la kisasa la kuogelea.
Hayo yalisemwa na rais wa FINA, Husain Al Musallam katika kongamano la kimataifa la mchezo wa kuogelea lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwl Nyerere hivi karibuni.
Al Musallam alisema kuwa wamevutiwa na vipaji vya wachezaji wa Tanzania katika mchezo wa kuogelea na ndiyo maana ameichagua nchi hii kuwa ya kwanza kuitembelea katika bara la Afrika tangu aingie madarakani.
Alisema kuwa amekutana tayari na viongozi wa TSA pamoja na serikali na kinachotakiwa sasa ni ushirikiano wa pamoja kufanikisha zoezi la ujenzi wa bwawa hilo.
“Naomba nieleweke wazi, kazi ya kuendeleza mchezo wa kuogelea si ya FINA peke yake, kuna serikali, vyama na wadau. Kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania, chama cha kuogelea na wadau, naamini tutafaniikisha ujenzi huu,” alisema Al Musallam.
Alisema kuwa FINA inataka kuona kuwa muogeleaji anashiriki mchezo huu bila kuwa na changamoto na kufanya vyema katika mashindano mbali mbali.
“Pia tunataka kuona mchezaji anakuwa na afya njema mara anapoamua kustaafu. Hii itamsaidia kuendelea kuupenda mchezo na kuwahamasisha wengine. Naomba niweke wazi, Tanzania ni moja ya nchi zilizopiga hatua ya maendeleo katika mchezo pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali, tumevutiwa sana na hili,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo nchini, Yusuph Singo alisema kuwa serikali imefarijika na ujio wa FINA na tayari wameonyesha mchoro na eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la kuogelea la kisasa la mita 50.
“Kwanza ujio wa rais wa FINA na viongozi wengine wakubwa wa shirikisho hilo ni heshima kubwa kwa nchi. Hakuna nchi ya Afrika ambayo imepata ujio mkubwa kama huu kihistoria na Tanzania imekuwa ya kwanza. Kama serikali tumefarijika sana na tunawapongeza TSA kwa kazi kubwa waliyoifanya,” alisema Singo.
Mwenyekiti wa TSA, Imani Alimanya alisema kuwa wamewasilisha mipango yao kwa FINA kuhusiana na maendeleo ua mchezo na wanaamini watafanikiwa.
Alimanya alisema kuwa moja ya mipango yao ni kuifanya Tanzania kuwa kituo kikuu cha mafunzo yamchezo wa kuogelea (High Performance Training Centre).
Kwa upande wake, rais wa kanda ya tatu ya mashirikisho ya kuogelea Afrika (CANA Zone 3), Donald Rukare aliipongeza FINA kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi pekee katika ukanda wake kuitembelea na kuhamasisha mchezo wa kuogelea.
Mbali ya Al Musallam, maofisa wengine wa ngazi za juu na rais wa Afrika wa mchezo huo, Sam Ramasamy.
Ramasamy pia ni makamu rais wa FINA mbali yakuwa rais wa Afrika wa shirikisho la mchezo huo (CANA) pamoja na Brent John Nowicki ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa FINA.
Wengine katika msafara huo ni Chaykh Ahmad Al Saab ambaye msaidizi wa rais wa FINA, Alex Szanto (FINA jumbe), Mikolaus Schonfeldt (msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa FINA) na bingwa wa zamani wa Olimpiki Ferry Weertam na Ranom Kromowidjojo ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia na Olimpiki.
Rais wa shirikisho la kuogelea la Kimataifa (FINA) , Husain Al Musallam (wa pili kushoto mstari wa nyuma) katika pozi na waogeleaji chipukizi kwenye bwawa la kuogelea la Champion Rise. Wengine katika picha ni mwenyekiti wa Chama cha kuogelea Tanzania, Imani Alimanya (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa FINA Brent John Nowicki, Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo (Yusuph Singo), rais wa Cana Kanda ya tatu, Donald Rukare na rais wa Shirikisho la kuogelea la Afrika Sam Ramasamy na Mjumbe wa Cana Kanda ya tatum Thauria Diria.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...