Na Eleuteri Mangi-WUSM, Dodoma
Macho na masikio ya watanzania, wapenda muziki na dunia nzima siku ya Jumamosi na Jumapili Machi 12 na 13, 2022 yatakuwa jijini Dodoma kuserebuka kwa Tamasha la Muziki la Serengeti ambalo linaratibiwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini.
Tamasha hili limekuwa nyenzo adhimu ya umoja na mshikamanao kwa wasanii wote nchini lenye kuleta tija kwa tasnia ya muziki na taifa ambapo wasanii wanapata jukwaa la kuonesha talanta zao na kuburudisha jamii hata kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa.
Ikumbukwe, tamasha hili linafanyika kwa miaka wa mitatu mfululizo ambapo kwa mara ya kwanza lilifanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam Desemba 2021 na mara ya pili ikafanyika jijini Dodoma Februari 2021 katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma na 2022 linafanyika tena jijini Dodoma.
Makala hii inajikita kwenye tamasha ambalo limekuwa kivutio kwa wapenzi wa muziki nchini na dunia kwa ujumla kwa kupata burudani ambayo inaenda sanjari na kutangaza fursa za utalii ambazo zipo hapa nchini.
Tamasha la Musiki la Serengeti limekuja na mbinu ya kuimarisha kazi ya Sanaa kuanzia kuibua vipaji vya wasanii, kuendeleza na hatimaye kuwa njia maridhawa ya kutangaza vivutio vya utalii ikiwemo utalii wa kiutamaduni hatua inayoingizia taifa mapato kutokana na hazina ya utalii vilivyopo hapa nchini.
Hili ni tamasha kubwa nchini linaloratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuibua na kusherehekea hazina ya vipaji vya wasanii wa kizazi kipya wa sasa na wazamani hatua inayoleta umoja na mshikamano miongoni mwa wasanii hao.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa anaweka bayana kuwa tamasha la Serengeti Music Festival mwaka 2022 litafanyika kwa siku mbili kuanzia Machi 12-13, 2022 jijini Dodoma tofauti na hapo awali ambapo lilipangwa kufanyika kwa siku moja. Hatua hiyo inatokana na mahitaji makubwa ya wasanii na wananchi kuhitaji kupata burudani pamoja pia nafasi ya kuonesha vipaji vya wasanii hapa nchini.
Ili kuleta hamasa na mvuto kwa wakazi wa Dodoma, mikoa jirani pamoja na dunia nzima, Mhe. Mchengerwa anasisitiza kuwa tamasha hilo litahusisha wasanii zaidi ya 50 wa muziki wa aina mbalimbali inayoleta vionjo na ladha tofauti tofauti ambao watashamirisha na kutumbuiza wasikilizaji na watazamaji kupitia njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo TV, redio na mitandao ya kijamii.
Akizungumza na Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo Machi 1, 2022 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi amesema kuongezeka kwa siku hizo mbili za tamasha jijini Dodoma inatokana uhitaji wa wasanii wengi kuomba kushiriki tamasha la mwaka huu.
“Mwitikio wa wasanii tulioupata katika msimu huu ni mkubwa sana, hadi sasa wasanii wakongwe na chipukizi zaidi ya 100 wameomba kushiriki tamasha hili kutokana na jinsi ambavyo limekuwa likiandaliwa vizuri na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Hili ndiyo tamasha pekee kubwa linalowaleta pamoja wasanii mbalimbali, wachanga na wakongwe, pia bendi za muziki zitajumuika pamoja bila kujali lebo zao” amefafanua Dkt. Abbasi.
Viongozi hao wakuu wa Wizara, Waziri Mhe. Mchengerwa pamoja na Katibu Mkuu wake Dkt. Abbasi wanathibitisha kuwa wamelipa tamasha hilo hadhi ya Serengeti ambayo ni mbuga bora Afrika na duniani.
Lengo likiwa ni kuonyesha na kurithisha Sanaa ya muziki kwa kizazi cha sasa na baadaye, kuitangaza nchi na vivutio vyake vya utalii kupitia Mbuga ya Serengeti ili kuwavutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kujionea vivutio hivyo hapa nchini na hatimaye taifa kuingiza fedha za kigeni na kutoa mchango kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Hakika Tamasha la Muziki la Serengeti ni darasa kwa wasanii tofauti na matamasha mengine ambapo wasanii wote wanaoshiriki wanapata fursa ya kufundishwa na wataalam mambo mbalimbali kulingana na kazi yao, kiuchumi na kijamii kabla ya kufanya maonesho yao ili kufikia lengo la tamasha hilo.
Ndiyo maana Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambao ndio Makao Makuu ya nchi Mhe. Anthony Mtaka, Machi 4, 2022 amefafanua kuwa tamasha hilo la Muziki ni kubwa na la kihistoria ambalo litawakutanisha wasanii zaidi ya 100 wa muziki ambao watakuja mkoani humo na kuhitaji mahitaji mbalimbali.
Amewahimiza wakazi wa jiji la Dodoma kuchangamkia fursa hiyo ambapo amewasisitiza kunufaika kiuchumi kwa kuwauzia bidhaa na kuwapatia huduma za kijamii wageni watakaokuja kwenye tamasha hilo.
“Tunaishukuru Serikali yetu kwa kutusogezea wimbi la wasanii zaidi ya 100 kwa mara moja kwa kuwa tunakwenda kunufaika sana. Huu ni utalii wa kiutamaduni na kiuchumi, shime wanadodoma tutumie fursa hii adimu” ameongeza Mhe. Mtaka.
Hii ni fursa adhimu ya ubunifu kwa Watanzania na dunia ambayo imeandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo inawaleta pia wanachi kushuhudia vionjo na ladha mbalimbali za muziki kutoka kwa wanamuziki nguli nchini ambao wanaipeperusha bendera ya Tanzania duniani kwa muziki wa bongo fleva, kughani mashairi, nyimbo za dini, taarabu na muziki wa singeli.
Tamasha la Muziki la Serengeti ni jukwa na kimbilio maridhawa kwa wasanii wote nchini bila kijali umri na ukubwa wao katika tasnia ya Sanaa, linawaleta katika jukwaa moja kuanzia wasanii wa kizazi cha zamani, kati na kizazi cha sasa ambalo ni jukwaa la Wizara kuwaratibu wasanii ili kukuza kazi zao.
Msanii Mrisho Mpoto maarufu kama Mjomba ni msanii nguli wa mziki wa dansi na Sanaa ya jukwaani hughani katika mziki wenye mahadhi ya Kitanzania anasema hana neno zuri la shukrani la kuipa Serikali iliyopo madarakani pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwani imewaheshimisha wasanii na kuwaleta wote kwenye jukwaa moja kupitia tamasha la muziki la Serengeti.
Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa
Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi akiwa pamoja na msanii wa kizazi kipya Faridi kubanda (FID Q) wakionesha nembo ya Tamasha la Muziki la Serengeti la 2022 ambalo litafanyika mwezi Machi 2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...