Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Said Mndeme akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na utaratibu wa kuhamia kwa wakazi watarajiwa wa nyumba hizo, leo jijini Dar es Salaam.
* Makabidhiano ya nyumba Magomeni Kota kuanza Jumatatu
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA,) imefanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan Machi 23 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota juu ya wakazi hao kununua nyumba hizo kwa utaratibu wa mpangaji- mnunuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika nyumba za makazi Magomeni Kota leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa TBA, Said Mndeme amesema katika uzinduzi huo Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ambapo Wakala hiyo iliyapa uzito na kuyafanyia kazi kwa haraka.
"Moja kubwa lililoelekezwa na Mh. Rais ni kuridhia wakazi wa nyumba hizi kuuziwa nyumba kwa utaratibu wa mpangaji-mnunuzi kwa kuzingatia hali zao za maisha kwa kurejesha gharama za nyumba pekee bila gharama ya thamani ya ardhi na miundombinu ya jumuiya ikiwemo maeneo ya kordo, lift na maeneo ya nje.'' Amesema.
Amesema wakala hiyo imefanyia kazi maelekezo hayo kwa kufanya ukokotozi wa gharama hizo na kukamilisha na taratibu zinazofuata ni za kiserikali ikiwemo kupata vibali na baadaye gharama hizo kutolewa kwa wahusika.
Mndeme amesema, zoezi hilo halitaathiri taratibu za makabidhiano na kuanza kwa matumizi ya nyumba hizo na mchakato wa makabidhiano hayo utaanza Jumatatu kwa wakazi 144 ambao wamepangwa katika ratiba wataanza mchakato wa kuhamia katika makazi hayo
"Tayari tumeweka utaratibu mzuri wa kuhamia kwa wakazi wa hapa na si kwa kupewa funguo... Kutakuwa taratibu za makabidhiano kuna fomu maalum zinazohusisha hali zote za nyumba na baada ya wakazi kuzikagua na kuridhika watasaini na maafisa wa TBA pia watasaini na watapewa pia barua za ofa zinazoonesha wamepewa nyumba hizi kwa utaratibu wa mpangaji-mnunuzi." Amesema.
Amesema, watakuwa na ofisini hapo katika kuhakikisha zoezi hilo linaenda kwa haraka na wakazi watarajiwa wanakabidhiwa nyumba hizo kwa wakati.
Aidha kuhusiana na utunzaji wa mradi huo Mndeme amesema Kutakuwa na na wataalam wa umeme na mabomba wakati wote pamoja na wafanyakazi wa idara ya Miliki kutoka Wakala hiyo watakaokuwa wanasimamia nyumba hizo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...