Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miliki kutoka TBA, Said Mndeme akizungumza na waandishi wa habari juu ya utaratibu wa wakazi wa Magomeni Kota kuhamia katika makazi hayo kuanzia jumatatu.


Na Lilian Lundo – MAELEZO

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) inatarajia kuanza kugawa nyumba kwa waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota kuanzia Machi 28, 2022.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miliki TBA, Said Mndeme leo Machi 25, 2022 katika viwanja vya Magomeni Kota, Jijini Dar es Salaam.

“Kwa sababu zoezi la ugawaji nyumba ni refu, hivyo tutaanza na wakazi 144 ambao tayari wamepangwa kwenye ratiba. Siku ya Jumatatu wakazi hao watakabidhiwa nyumba, ambapo nyumba moja baada ya nyingine itakaguliwa. Mkazi husika atatakiwa athibitishe kila kifaa katika nyumba atakayokabidhiwa kiko sawa,” alifafanua Mndeme.

Aliendelea kusema kuwa, zoezi hilo litahusisha kuangalia kifaa kimoja baada ya kingine kama vile milango, madirisha pamoja na rangi. Aidha, mpangaji mnunuzi atakagua mwenyewe nyumba,  na ikiwa ataridhika na hali ya nyumba, atasaini  na kwa upande wa TBA Afisa atakayekuwa anakabidhi nyumba hizo atasaini, na rasmi nyumba hizo zitakuwa zimekabidhiwa pamoja na funguo.

Mndeme amesema kuwa, wamejipanga vyema kufanya zoezi hilo, ambapo ofisi za TBA zitakuwepo eneo hilo la Magomeni Kota ili kuhakikisha zoezi la ugawaji nyumba linaenda kwa utaratibu mzuri na kuhakikisha kuwa, watu wanaofika eneo hilo ni watu wanaotakiwa kupewa nyumba kwa siku husika kulingana na ratiba iliyopangwa.

Vilevile ameeleza kuwa, TBA imeanza kufanyia kazi maelekezo ya Mhe. Rais Samia baada ya kutoa ridhaa ya wakazi  644 wa Magomeni Kota kuuziwa nyumba hizo kwa utaratibu wa mpangaji mnunuzi kwa kuzingatia hali zao za kimaisha ambapo Mhe. Rais alitoa maelekezo kwamba gharama watakazopewa zihusishe nyumba peke yake bila kuhusisha thamani ya ardhi pamoja na miundombinu ya jumuiya kama vile korido, maeneo ya lifti na maeneo ya nje.  

“TBA tumeshakamilisha ukokotozi wa gharama za nyumba hizo na taratibu zinazofuata ni za kiserikali kwa maana ya kupata vibali na taratibu nyingine, na gharama hizo wataanza kupewa wahusika. Mikataba ya mauzo ya nyumba za serikali iko rafiki, ambapo mnunuaji anapendekeza mwenyewe atakavyolipa gharama hizo kwa kipindi cha miaka kumi kutokana na uwezo wake,” alifafanua Mndeme.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...