Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
WAFANYABIASHARA wadogo wadogo wameshauriwa kuacha kuingiza bidhaa za magendo zinazopitishwa katika njia zisizohalali ili kuepuka madhara ya kiafya na kiuchumi kwa Tanzania na mtu binafsi.
Hayo yamesemwa na Ofisa Msimamizi wa Kodi Mkoa wa Kilimanjaro Odupoi Papaa wakati wa utoaji elimu kwa wafanyabiashara wa mipakani kuhusu athari za biashara za magendo kutoka TRA makao makuu iliyofanyika katika mpaka wa Kenya na Tanzania wa Holili.
Amesema madhara ya bidhaa hizo yameanishwa katika maeneo matatu ikiwemo Afya ya walaji, kutokana na kutumia bidhaa ambazo zimeisha muda wake wa matumizi.
"Kumekuwepo na baadhi ya watu ambao wanabadilisha bidhaa kwenye mifuko mipya ikiwa bidhaa hizo zimekwisha muda wa matumizi,hivyo kusababisha madhara makubwa kwenye afya zetu.Tukatae bidhaa za magendo"amesema Papaa.
Aidha amewataka wananchi hao kuacha kutumia bidhaa za magendo kutokana na athari kubwa zinazopatikana katika bidhaa.Hivyo amewakumbusha wahakikishe bidhaa zinazopita katika njia halali ziwe bidhaa salama kwa afya ya walaji.
"Madhara mengine yanayopatikana ni kwa nyinyi wenyewe kukamatwa na bidhaa za magendo ambapo madhara yake ni makubwa ikiwemo kupigwa faini na kupelekea jela,"amesema Papaa.
Kwa upande wake, Ofisa Mfawidhi Kituo cha Forodha Holili Yusuph Mwahu amewashauri wafanyabiashara wadogo wadogo kupitia lango Kuu kwani barabara ipo vizuri na ushuru ni wa kawaida na wameweka dirisha malumu kwa ajili ya kulipa ushuru kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu.
Amesema hakuna sababu wafanyabiashara hao kupita porini kwa lengo la kukwepa kodi kwa kupitisha bidhaa za magendo bali wapite lango kuu la Holili.
Sambamba na hayo, amekitaka kitengo cha elimu kwa mlipa kodi cha TRA kuendelea kutoa elimu mara kwa mara hasa sehemu za mipakani Ili uwelewa uwe mkubwa zaidi kwa jamii.
Wakati kwa Mkaazi wa Holili Abdul Abdul ambaye awali alikua akifanya biashara ya magendo amesema baada ya kupata elimu ameacha kazi hiyo na anapita katika lango kuu, hivyo amewataka maofisa wa RTA waendelee kutoa elimu Ili watu wengi wawe na uelewa kuhusiana na athari za kupitisha bidhaa za magendo.
"Nawaomba maofisa wa forodha mnaozunguka nchi nzima katika kutoa elimu ya mlipa kodi muhakikisha elimu hii inawafikia watu wote, kwani kuna baadhi ya watu wanadhani kuna bidhaa ambazo haziruhusiwi kupita katika lango kuu jambo ambalo sio sahihi kwani bidhaa zote zikishakaguliwa zinaruhusiwa kupita,"amesema Abdul.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...