Na Chalila Kibuda michuziTV
ZAIDI ya shilingi Trilioni 25 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kwa vipande vya Dar es Salaam Kigoma na Dar es Salaam pamoja Mwanza
Akizungumza na waandishi habari Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa wakati Kamati ya Bunge ya Bajeti ilipotembelea mradi wa reli ya kisasa toka stesheni hadi Soga mkoani Pwani.
Kadogosa amesema ujenzi huo unatumia fedha za ndani pamoja na mikopo mbalimbali kutoka taasisi za fedha na kwamba Sh bilioni 600 imeshatolewa kwa mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha Makutupora Dodoma hadi Tabora.
Amesema ujenzi wa reli kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro ulitumia fedha za ndani na mikopo mbalimbali kutoka Denmark na Sweden ambayo ilikuwa na riba ya asilimia tatu ambapo ni mkopo nafuu na ulipaji ni muda mrefu.
"Mkopo huu ni wa miaka 20 na zaidi na ni mkopo mzuri sana kwani ulitupa fursa ya kufanya majadiliano. Upembuzi yakinifu kuhusu mradi huu ulifanywa na serikali ya awamu ya nne na serikali nyingine zimeendeleza," alisema Kadogosa.
Alisema katika mradi huo hawatategemea mizigo pekee kujiendesha badala yake itashirikisha sekta binafsi kwa ajili ya kuanzisha huduma za kifedha, migahawa na biashara ambazo zitawaongezea mapato.
"Ni lazima reli ijiendeshe kwa kutumia mapato mbalimbali yatakayokusanywa kutoka katika vitega uchumi tulivyoviweka kwenye vituo vyetu vyote vya abiria," alisisitiza.
Alisema wakikamilisha ujenzi huo kwa kuunganisha maeneo muhimu ya bandari itachukua miaka 15 kupata faida na kwamba wanafanya jitihada mbalimbali kurudisha mzigo mkubwa unaochukuliwa Uganda kuliko nchi zote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Daniel Sillo alisema serikali imefanya kazi kubwa katika mradi huo wa Kilometa 300 na kwamba asilimia kubwa imekamilika (95.3).
Alisema reli ni muhimu kwa uchumi na kijamii na kwamba ni mradi muhimu kwa maendeleo ya nchi hivyo, wanaamini wataishauri vyema serikali katika utendaji kazi.
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete alisema tayari Sh trilioni 14.5 zimeshalipwa kwa mkandarasi na kwamba Sh trilioni saba niza mikataba mbalimbali hivyo, wanaamini katika bajeti ijayo itawasaidia kutekeleza miradi kwa wakati ili kutoa huduma bora kwa jamii.
Alisema wameagiza behewa 44 na vichwa vipya vitatu kwa ajili ya kupeleka mizigo katika bandari ya Isaka na kwamba wanatarajia kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa nchi za Rwanda, Congo, Burundi na Uganda ili kutumia fursa hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...