Na Mwandishi wetu, Roma
Ubalozi wa Tanzania nchini Italia umekutana na kufanya Mkutano Mkuu na Jumuiya mbalimbali za Watanzania wanaoishi maeneo mbalimbali nchini Italia (Diaspora) kwaajili ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya pande mbili.
Akifungua mkutano huo mwishoni mwa wiki, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo alitoa wito kwa Watanzania hao kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuiletea Tanzania maendeleo.
“Nawashauri kujisajili katika daftari la Diaspora wa Italia ili kuwa na takwimu na kumbukumbu sahihi za Watanzania waliopo Italia. Takwimu na kumbukumbu hizi zitasaidia Ubalozi kuwaunganisha Wanadiaspora na wabia wa maendeleo ambao wana nia au tayari wanaendesha shughuli zao nchini Tanzania na wanahitaji kushirikiana na Diaspora,” Amesema Balozi Kombo.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulijadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanadiaspora ikiwemo changamoto za kiutendaji na ushirikiano katika Jumuiya zao ambazo zilianishwa wazi kwenye taarifa za kiutendaji zilizowasilishwa na Viongozi wa Jumuiya.
Mkutano uliazimia kuendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya Wanadiaspora na Ubalozi kwa kuanisha mkakati thabiti wa kuboresha mawasiliano baina ya pande mbili.
Aidha, wanadiaspora hao wameahidi kuendelea kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia katika kuiletea nchi yao maendeleo kwa kuwekeza nchini kwao. Kadhalika, Ubalozi umeahidi kutafuta suluhu ya kudumu dhidi ya changamoto zinazowakabili wanadiaspora waishio nchini Italia.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na wanadiaspora takriban 100 akiwemo Mhashamu Baba Askofu Mkuu Protase Rugambwa, Katibu Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.
Nchini Italia zipo Jumuiya sita zinazotoka maeneo ya Roma, Napoli, Modena Central North, Genova, Modena na Umoja wa Watanzania Wakatoliki unaojumuisha Waklero, Watawa, Waseminari na walelewa wa Utawa wanaofanya kazi za kitume hapa Italia.
Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akiongea na Wanadiaspora (hawapo pichani) wanaoishi nchini Italia wakati wa Mkutano
Katibu wa Jumuiya ya Watanzania Roma akiwasilisha Bi. Anastacia Lubangila, taarifa ya Jumuiya hiyo wakati wa mkutano
Mhashamu Baba Askofu Mkuu, Protase Rugambwa akifuatalia majadiliano
Mwenyekiti Kamati Kuu ya Wanadiaspora Italia Bw. Maulid Kagutta, akiwasilisha taarifa ya Diaspora Italia
Balozi Kombo akipokea picha ya nembo rasmi ya Jumuiya ya Watanzania Genova kutoka kwa Bi. Eva Nangela, Mwenyekiti wa Jumuiya (kushoto). Wanaoshuhudia (kulia) ni Bi. Zakia Kombo, Mwenza wa Mhe. Balozi; Baba Askofu Mkuu Rugambwa na Maafisa Ubalozi, Bw. Sigfried Nnembuka pamoja na Jacqueline Mbuya.
Wanadiaspora wakifuatilia mkutano
Wanadiaspora wakifuatilia mkutano
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...