Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis(wa tatu kushoto) akionesha nakala ya Taarifa ya utafiti wa Hali ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni baada ya kuzindua taarifa hiyo jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/2022
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizungumza wakati wa uzinduzi wa   Taarifa ya utafiti wa Hali ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni na kuizindua  rasmi taarifa hiyo jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/2022.


WATOTO wapatao laki mbili wamekumbana na ukatili wa kingono mtandaoni kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika mwaka 2020 huku sababu kuu ikiwa ni matumizi mabaya ya vifaa vya kielektroniki na mitandao ya kijamii kwa kundi la watoto linalofikia asilimia nne.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaid Ally Khamis wakati wa uzinduzi wa taarifa ya utafiti kuhusu hali ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni Tanzania na kueleza kuwa matumizi ya vifaa vya kielektroniki na mitandao ya kijamii wakati wa mlipuko wa UVIKO-19 licha ya kuleta manufaa katika mawasiliano na ujifunzaji kwa wanafunzi kupitia mtandao bado kundi la watoto hasa vijana balehe wamekumbana na ukatili wa kingono kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Instagram na WhatsApp.

Naibu Waziri Mwanaidi ameeleza kuwa taarifa ya utafiti wa Ukatili dhidi ya Watoto Mtandaoni uliofanyika mwaka 2018 na Mtaalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dkt Hezron Onditi inaonyesha kuwa asilimia 4 ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 17 walifanyiwa ukatili wa kingono ikiwemo kulazimishwa kutoa picha zao za utupu.

Ameongeza kuwa amefarijika kupata taarifa ya hali ya ukatili wa kimtandao katika kipindi hiki ambapo tumeanza kushuhudia watoto wameanza kupata madhara yanayotokana na ukatili wa kimtandao nchini hivyo itasaidia kuongeza afua zaidi za kupambana na ukatili mtandaoni ambao unaenea kwa kasi.

Amesema, utafiti huo uliofanywa na Wizara kwa kushirikiana na watafiti wakuu wa Shirika linaloshughulikia masuala ya watoto duniani (UNICEF,) Shirika la Kupambana na Ukatili wa Kingono kwa Watoto (ecpat,) na Shirika la kuzuia uhalifu duniani (INTERPOL,) pamoja na wadau wengine umebaini kwamba wahusika wanaofanya ukatili wa kingono kupitia mitandao ni watu wa karibu wa watoto hao ambao wamekuwa wakitoa taarifa hizo kwa marafiki badala ya vyombo husika wakiwemo polisi, wazazi pamoja na madawati ya jinsia.

Aidha amesema, Serikali itaendelea kuimarisha mifumo yote ya ulinzi na usalama wa mtoto kama ilivyoelekezwa katika mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu haki na ustawi wa mtoto ili kuhakikisha hakuna mtoto anayefanyiwa vitendo vya ukatili.

Amesema taarifa hiyo imebainisha masuala muhimu ya kuwalinda watoto ambayo wadau kuanzia ngazi ya familia wanatakiwa kushiriki kwa kuimarisha ulinzi kwa watoto na kufahamu madhara ya vitendo hivyo kwa watoto.

''Serikali itaweka Sera ambayo wadau walio tayari wanaweza kushiriki katika vita kwa pamoja kukomesha vitendo hivi.....Namwelekeza Mkurugenzi wa Idara ya Watoto kusimamia mikakati hii pamoja na kuwashirikisha wadau wengine walio tayari kushiriki na sio kubaki na taarifa hizi katika mafaili yenu.'' Amesema.

Kuhusiana na elimu kwa Umma kuhusiana na vitendo vya ukatili kwa watoto mitandaoni Naibu Waziri Mwanaid amesema Wizara inaandaa majarida mahususi kwa wazazi, walezi, walimu, wadau na watoto wenyewe kuhusiana na vitendo hivyo na namna ya kuripoti na kukabiliana navyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Watoto Sebastian Kitiku amesema kuwa utafiti huo ulilenga kuangalia aina za ukatili wa watoto mitandaoni, madhara na hatua stahiki za kuchukua katika kukomesha hilo na kwa kushirikiana na wadau wamekuja na taarifa hiyo iliyopelekea kuwakutanisha wadau hao kwa hatua za utekelezaji.

“Utafiti umetumia mbinu mbalimbali kama uchambuzi wa Sera na Sheria zilizopo Nchini ,Upitiaji wa nyaraka mbalimbali mitandaoni,Mahojiana na Watoto na Wazazi kwa ujumla Pamoja na Mikusanyiko mbalimbali kwa kushirikiana na ngazi za kata hadi mkoa.”amesema Kitiku.

Amesema Wizara kwa kushirikiana na watafiti wakuu wa Shirika linaloshughulikia masuala ya watoto duniani (UNICEF,) Shirika la Kupambana na Ukatili wa Kingono kwa Watoto (ecpat,) na Shirika la kuzuia uhalifu duniani (INTERPOL,) pamoja na wadau wengine walitafiti suala hilo baada ya kuongezeka kwa hali ya ukatili wa watoto katika mitandao hali inayokuja kasi kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii na kuukamilisha Desemba 2021.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la UNICEF Shalini Bahguna ameipongeza Serikali kwa kuweka juhudi za msingi za kupinga vikali ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto hasa katika jitihadaz.a kupambana na ukatili mtandaoni.Amesema Shirika hilo limejikita katika kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama na kuhakikisha watoto wanajengewa uwezo wa kujitambua ili kuepukana na ukatili wa mtandaoni na kuiomba Serikali kuendelea kutoa ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuondoa tatizo la Ukatili mitandaoni.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watoto Nancy Kasembo ameshukuru kwa kushirikishwa kwao katika michakato inayowahusu watoto kwani ina manufaa kwao na kuiomba jamii kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa watoto katika mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

“Watoto hawajui namna ya kutoa taarifa baada ya kufanyiwa ukatili,aidha bado kuna unyanyapaa dhidi ya wahanga wa ukatili hivyo kupelekea wahanga kutotoa taarifa”. amesema Nancy.

Baadhi ya wadau wakichangia umuhimu wa utafiti huo wamesema ni vema kuwekeza kwenye kuweka mbinu zinazozuia watoto kufanyiwa ukatili wa mitandaoni kabla haujatokea na hiyo ni kwa mbinu kama kuzuia na kuwakataza watoto kujihusisha na baadhi utumiaji wa mitandao kama watu wazima.

Aidha, wameiomba Serikali kutenga bajeti na kuwajengea uwezo watoa huduma hususani kwenye madawati ya kijinsia na Polisi na kuwaasa wazazi na walezi kujadili masuala ya msingi yanayowahusu watoto wao ili kuwajengea ukaribu na watoto waweze kusema pale wanapofanyiwa ukatili.

Utafiti huo umeonesha kwamba mwaka 2020 pekee watoto laki mbili wenye umri wa miaka 12 hadi 17 walipitia changamoto ya ukatili wa kingono kwa kuchapishwa kwa picha zao za utupu bila ridhaa na video za utupu kwa ahadi za zawadi.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake ma Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akitoa kwa baadhi ya wadau, nakala ya taarifa ya utafiti kuhusi hali ya ukatili mtandaoni dhidi ya watoto, baada ya kuizindua taarifa hiyo, jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/0/2022.
Mwakilishi wa Shirika la umoja wa Mataifa la Unicef Shalini Baghuna akitoa  maelezo kuhusu taarifa ya utafiti kuhusu hali ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni wakati wa uzinduzi wa taarifa hiyo uliofanyika jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/2022.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Sebastian Kitiku akieleza lengo la uzinduzi wa Taarifa ya utafiti wa hali ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni, jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/2022.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake ma Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akitoa kwa baadhi ya wadau, nakala ya taarifa ya utafiti kuhusi hali ya ukatili mtandaoni dhidi ya watoto, baada ya kuizindua taarifa hiyo, jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/0/2022.

Baadhi ya washiriki wa hafla ya uzinduzi wa taarifa ya utafiti kuhusu hali ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni wakifuatilia matukio mbalimbkai katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/2022.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...