WADAU wa haki za wanawake Pemba wameiomba serikali kufanyia marekebisho baadhi ya sheria zinazokwaza ufikiaji wa usawa wa kijinsia kwa wanawake ili kuwezesha ushiriki sawa wa kijinsia katika fursa mbalimbali.

Hayo yametolewa kwa nyakati tofauti wakati wa mdahalo wa wadau uliolenga kujadili changamoto za kisheria zinazowakwaza wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi katika Wilaya za Micheweni, Wete, Chake chake na Mkoani Pemba ulioandaliwa na taasisi ya PEGAO kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar) ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.

Walisema uwepo wa sheria hizo Zanzibar unarejesha nyuma juhudi za wanawake kujitokeza kushiriki katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

Safia Saleh Sultan, mwanasheria kutoka kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, (ZLSC), alitaja baadhi ya sheria zinazokwaza ushiriki wa wanawake katika uongozi kuwa ni; Sheria ya watumishi wa Umma No.3/2003, Sheria ya Mahakama ya Kadhi No.7/2001, Sheria ya Vyama vya Siasa (1992) na Sheria ya Uchaguzi no 4/2018, ambapo sheria hizo zimeweka masharti magumu kwa wanawake wanapohitaji kugomea nafasi za uongozi.

Alisema kutokana na masharti ya sheria hizo kuwa ngumu kwa wanawake watumishi wa umma inapelekea kukosekana kwa wanawake wenye uwezo mzuri wa kiutendaji katika ngazi za maamuzi.

“Wanawake wengi wanaofanya kazi Serikalini na walio na uwezo mzuri wanaogopa kuingia kugombea nafasi za siasa na kuitumia haki yao ya msingi ya kikatiba kwa kuhofia kupoteza nafasi zao kazini kutokana na masharti ya kisheria kuwa magumu,” alieleza.

Alieleza wakati dunia ikiwa katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ni muhimu kuongeza ushawishi wa maboresho ya sheria hizo ili zitoe fursa kwa makundi yote kushiriki kaika nafasi za uongozi bila vikwazo.

Alisema, “tukiwa kama ni wadau wakuu wa maswali haya ya kutetea haki za wanawake na uongozi na wadau wa Sheria, ni vyema sote kwa pamoja tukashirikiana kuhakikisha kwamba kwamba Sheria hizi zinafanyiwa utetezi wa maboresho ili ziweze kukidhi misingi ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini.”

Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib, alisisitiza wanawake kutumia maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kutahimini changamoto zinazowakwaza katika nyanja mbalimbali na kuzitumia kuwa fursa ya kufikia ukombozi wa mwanamke.

“Kuelekea siku ya wanawake duniani, sisi wanawake tunatakiwa kujitathimini kwa zile changamoto ambazo zinatukwaza kufikia malengo yetu na tuzigeuze kuwa fursa ya kufikia upatikanaji wa haki zetu na sio kulaumiana,” alisema Salama.

Sabahi Musa Said, mshiriki wa mdahalo huo alisema ili kufikia ushiriki sawa wa wanawake katika nafasi za uongozi ni lazima kuwepo kwa sheria zinazolazimisha usawa wa kijinsia katika kila nafasi.

Alieleza, “kuwepo kwa sheria lazimishi kuhusu usawa wa kijinsia kwa wanawake kushiriki katika kila nafasi za uongozi ndiyo itasaidia kufikia lengo la asilimia 50% katika ngazi zote.”

Kwa upande wake Hasina Ibrahim, mwanachama wa chama cha Mapinduzi CCM alishauri kufanyiwa marekebisho ya ukomo wa miaka kwa wabunge na wawakilishi ili kutoa fursa zaidi kwa wengine kushiriki nafasi hizo.

“Ikiwa rais anawekewa ukomo wa miaka 10 kwanini mbunge anaongoza maisha.? Wawakilishi na wabunge wakishakaa miaka 10 kama rais wasirudi wapishe wengine kwasababu Wanawake wengi tunashindwa kupita kwasababu ya rushwa kwa baadhi ya wabunge na wawakilishi kutumia nguvu na uwezo wao kifedha kushawishi wapiga kura,” alisema Hasina.

Nae Salma Haji Mcha, spika wa serikali ya wanafunzi katika shule ya Sekondari Uweleni, Wilaya ya Mkoani Pemba alisema Watoto wa kike kutokuaminiwa uwezo wao mapema katika nafasi za uongozi bado ni changamoto kubwa inayopelekea wanawake kushindwa kupewa fursa za uongozi.

Alieleza, “mwanzoni nilipoingia shule nilitaka nigombee urais lakini mmoja wa walimu akaniambia kabisa hata kama nikipata kura zote hawezi kunipitisha nikawa rais kutokana na mimi ni mwanamke.”

Aidha aliongeza kwamba ili kufikia usawa wa kijinsia jamii inahitajika kuwa na utayari wa kumuinua mwanamke katika kila fursa na si kumuangusha.

Mapema mkurugenzi wa PEGAO, Hafidh Abdi Said, alisema PEGAO kwa kushirikiana na TAMWA Zanzibar wameandaa midahalo hiyo kwa lengo la kujadili Pamoja changamoto kisheria zinazowakwaza wanawake ikiwa ni utekelezaji mradi wa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi unaofadhiliwa na Ubalozi wa Norway.

“Tukiwa tunaelekea siku ya wanawake duniani, tumekutana kwa lengo la kujadili changamoto za kisheria zinazowakwaza wanawake katika harakati za uongozi ili kuhakikisha tunapata kufikia suluhisho la usawa wakijinsia kwa kila nyanja,” Hafidh Abdi, Mkurugenzi PEGAO.

Katika mdahao huo uliofanyika kwenye wilaya Nne za Pemba, jumla ya Sheria tisa zinazokwaza ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi zimejadiliwa na wadau hao ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya Siku ya wanawake duniani yanayofanyika machi nane kila mwaka ambapo kauli mbiu ya wadau ni ‘Haki na Usawa wa Kijinsia katika Nafasi za Uongozi kwa Maendeleo Endelevu.’




Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba akizungumza wakati wa mdahalo

Mkurugenzi wa PEGAO, Hafidh Abdi Said akizungumza wakati wa mdahalo
mwanasheria kutoka kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, (ZLSC), Safia Saleh Sultan akiwasilisha mada wakati wa mdahalo.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...