Na Moses Mashalla,Arusha

MEYA wa Jiji la Arusha Maximillan Iranqe amewataka waganga wanaojishughulisha na tiba asilia mkoani Arusha kuwekeza zaidi katika tafiti za mimea inayotibu maradhi ya mbalimbali kama nchi za barani Asia hususani China.

Pia awashauri waganga hao kujiepusha na vitendo vya utapeli ili kuipa sifa na hadhi taaluma hiyo tofauti na inavyozungunzwa kwa sasa.

Akizungumza kwenye mkutano wa halmashauri kuu ya Chama Cha Waganga na wakunga wa Tiba asilia(Chawatiata) kilichofanyika katika ofisi za Ccm wilayani Arusha amewataka waganga hao kufikiria kuwekeza nguvu zaidi kwenye ubora wa dawa mbalimbali hususani mitishamba inayotibu maradhi mbalimbali.

"Fikirieni kuwekeza kwenye ubora wa madawa yenu hususani mitishamba kama wanavyofanya nchi za Asia kama China," amesema na huku akiwataka pia washiriki washiriki wa mkutano huo kuepuka vitendo vya utapeli na udanganyifu ili kuipa sifa taaluma hiyo.

Aidha amewashauri kuboresha mazingira ya maeneo wanayofanyia kazi pamoja na bidhaa wanazowapa wagonjwa."Lazima mjipambanue baina ya waganga wa kienyeji na tiba asilia acheni kufunga dawa kwenye magazeti lakini muwe smart(nadhifu)" amesema Meya Iranqe

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Kiondo Msangi amemwambia Meya huyo aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo kuwa chama chao mbali na kisajiliwa kisheria na kupewa leseni ya uendeshaji lakini wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu kutokana na baadhi ya wanachama kukamatwa hovyo na kutozwa adhabu kinyume na sheria.

Msangi amesema kuna kikundi cha baadhi ya watu kimekuwa kikizunguka mkoani Arusha na kuwashawishi na kuwapotosha wajumbe kutojiunga na chama hicho kutokana na sababu zao binafsi na kuiomba serikali kukichukulia hatua.

Wakati huo huo ,Katibu wa chama hicho ,Kifumba Mkombozi amesema kwamba chama chao kimekuwa kikishirikiana na serikali katika kuwafichua wapiga ramli chonganishi,majambazi na hata kukemea mauaji na watu wenye ulemavu wa ngozi na kuiomba serikali kuwaunga mkono.

Awali Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha (Mt Meru),Dk.Omary Chande ametoa rai kwa waganga hao kuhakikisha wanawakamata wale wanaofanya shughuli za tiba asilia bila leseni kwa kuwa hao ndio wanachafua taaluma hiyo.

Dk. Chande ameshauri waganga hao kuhakikisha wanashiriki kikamilifu na kuunga mkono na kuhamasisha zoezi la chanjo ya Uviko -19 linaloendelea nchini kwa kuwa wao wana nafasi kubwa ndani ya jamii.

 

Meya wa Jiji la Arusha Maximillan akizungumza kwenye Mkutano huo uliohusisha waganga wa tiba asili mkoani Arusha

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...