BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
WADAIWA sugu 400 wa kodi ya pango la ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela,wamefikishwa kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba, Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza,wakidaiwa sh.bilioni 4.2 za kodi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya baraza hilo,Kamishna wa Ardhi,Mkoa wa Mwanza,Elia Kamihanda, amesema wadaiwa hao sugu wa kodi ya serikali walifikisha leo kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba,Wilaya ya Nyamagana.
Amesema serikali imewafikisha mahakamani watu 400 kwa mujibu wa sheria ya ardhi kifungu cha 50 wakidaiwa kukaidia kulipa kodi ya ardhi kwa muda mrefu licha ya hatua mbalimbali za kuwakumbusha, kuwaelimisha umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati na kuwapatia ilani na hati za madai ya kodi wanayodaiwa.
“Tumeanza rasmi Leo kuchukua hatua za kisheria na kuwafikisha mahakamani wamiliki wa ardhi na wadaiwa sugu 400 ya kodi la pango la ardhi baada yakuvunja takwa la sheria, kifungu cha 50 cha sheria ya ardhi na kukaidi kulipa kodi ya miliki zao kiasi cha sh. bilioni 4.2,”amesema Kamihanda.
Amesema endapo mmiliki wa ardhi akishindwa kulipa kodi kamishna kwa mamlaka aliyopewa anawajibika kumfikisha mahakamani,hivyo mpango wa ofisi hiyo ni kuwafikisha mahakamani na kuwashitaki wote walioshindwa kulipa kodi kwa wakati licha ya kukumbushwa wajibu huo na kusistiza hata ambao hawakulipa kodi wanayodaiwa mwaka jana watashitakiwa.
Ameongeza kuwa suala la kuwafikisha mahakamani wenye milki za ardhi wasiolipa kodi halitaishia kwa Jiji na Manispaa ya Ilemela,litafanyika pia kwenye wilaya zote za Mkoa wa Mwanza na tayari ilani za kuwafikisha mahakamani zimeandaliwa kwa wadaiwa sugu wilayani Magu, wanaodaiwa sh. milioni 700 za kodi.
Kamishna huyo wa ardhi,amesema mwaka jana walikusanya maduhuri ya serikali yanayotokana na huduma mbalimbali ikiwemo kodi ya pango la ardhi sh. bilioni 8 kati ya bilioni 14 sawa na asilimia 70.
Amesema mwaka huu wa fedha wanalenga kukusanya sh.bilioni 18 za maduhuri ya serikali,changamoto kubwa inayowakabili ni wamiliki wa ardhi kutokuwa tayari kulipa kodi ya miliki zao.
Kamihanda amewataka wamiliki wa ardhi na wanaodaiwa kulipa kodi ya pango la ardhi wasisubiri kushitakiwa kwenye mabaraza ya ardhi kwani lengo la serikali ni kuhahakisha makusanyo yanapatikana ili kusaidia shughuli za maendeleo na kutekeleza miradi ya kimkakati.
“Suala la kulipa kodi ya pango la ardhi bila shuruti ni takwa la kisheria, tunawathamini wanaotii bila kusukumwa na sheria,na mkakati wa wizara ni kuwaelimisha wamiliki kabla ya kuwachukulia hatua za kisheria,rai yangu watu walipe kodi kwa wakati,ambao hawako tayari watachukuliwa hatua za kisheria,”alionya.
Ameeleza kuwa serikali ilishaweka jitihada zake za kutoa elimu kupitia kwa watendaji wa sekta ya ardhi,pia viongozi wa wizara hiyo wamekuwa wakichukua jukumu la kutoa elimu na kuwasistiza wananchi kutekeleza wajibu wao kisheria wa kulipa kodi,sasa jitihada hizo zinatosha.
Kamishna wa Ardhi, Mkoa wa Mwanza,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu wadaiwa sugu 400 wa kodi ya pango la ardhi kufikishwa mahakamani leo.Picha na Baltazar Mashaka
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...