Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amewapongeza viongozi wa kuu wa taifa kwa mikakati mbalimbali waliyoiweka ambayo imekifanya kiswahili kuwa lugha ya kimataifa.
Mhe. Mchengerwa ametoa pongezi hizo leo Machi 14, 2022 wakati akimkaribisha Makamu wa Rais. Mhe. Dkt. Philip Mpango kufungua Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Duniani 2022 jijini Arusha.
"Sisi wadau wa Lugha ya Kiswahili tunazipongeza kwa dhati jitihada za kukiendeleza Kiswahili zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan wewe Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa". Ameeleza Mhe. Mchengerwa
Amesema kuwa jitihada za viongozi hao zimekiwezesha Kiswahili, kutangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kuwa na siku yake rasmi kila mwaka, ambayo ni tarehe 7 ya mwezi Julai kila mwaka.
Ameongeza kuwa uamuzi huo ulitolewa wakati wa mkutano wa nchi wanachama wa Shirika hilo ambapo hatua hiyo inakifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na kuwa na siku yake maalum ya kuadhimishwa.
Aidha, amefafanua kwamba Kiswahili kimetangazwa kuwa lugha ya kazi ya Umoja wa Afrika, uamuzi uliopitishwa katika mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja huo, tarehe 6 Februari, 2022.
"Mwelekeo wenu wa kukiendeleza Kiswahili unatufanya sisi wadau wa Kiswahili kutembea ‘kifua mbele’. Ikumbukwe kwamba Kiswahili kimekuwa miongoni mwa lugha rasmi zinazotumika katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC tangu mwaka 2019". Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Kwa upande mwingine amesema wadau wa kiswahili wanaamini kuwa uamuzi mbalimbali ambao umekuwa ukifanywa kuhusu Lugha ya Kiswahili ni wa kizalendo na utawawezesha Watanzania na wananchi wa Afrika Mashariki kupata fursa za kushiriki katika shughuli za ukalimani, tafsiri, uhariri, uandishi na uchapishaji wa vitabu pamoja na fursa za kufundisha Kiswahili kwa wageni na hivyo kujipatia kipato.
"Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, kupitia Mabaraza yetu mawili ya BAKITA na BAKIZA tunaendele kutekeleza maagizo yanayohusiana na Lugha ya Kiswahili ya Rais na yaliyomo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020". Ameongeza
Kongamano hilo litakuwa la siku tano, Machi, 14-18, 2022 ambapo mada mbalimbali zitajadiliwa na idhaa nazo zitapata fursa ya kuelezea changamoto zao za matumizi ya lugha ya Kiswahili na kujadiliana kuhusu utatuzi wake.
Ameongeza kuwa maazimio yatakayowekwa katika Kongamano hili yatatekelezwa na BAKITA na BAKIZA chini ya usimamizi wa Wizara hizi mbili.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Yakubu Saidi amesema Kongamano hilo la kihistoria litatoa mchango mkubwa kwenye lugha ya kiswahili kwa kuwa limesheheni magwiji, magalacha na wabobezi wa fani za Uandishi na Utaalamu wa Lugha ya Kiswahili.
Viongozi wengine wa Serikali waliohudhuria Kongamano hilo ni Mhe. Tabia Maulid Mwita, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Zanzibar na Mhe. Pauline Gekul Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...