Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Tanga

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Tanzania Bara Kanali Mstaafu Abdulrhaman Kinana amesema Chama hicho lazima kisiimamie Serikali kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya wafanyabiashara wakiwemo Machinga na Mama Lishe kufanya shughuli zao bila kusumbuliwa na kuwekewa vikwazo.

Akizungumza mbele ya wana CCM Mkoa wa Tanga kwenye kikao cha ndani akiwa wilayani Korogwe, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Abdulrhaman Kinana amesema watanzania waliwachagua, wakaunda Serikali , ndio maana chochote kinachofanyika watakwambia ni CCM.

“Hivyo wakifika mahali wakaona mambo yako vile vile watachoka, niwaombe tuwe karibu na wananchi, tuwe sikio la wananchi , tuwasikilize wananchi wanataka nini hata kama wanachotaka hukipendi, lazima tuwasemee wananchi.

Amefafanua kwa muda mrefu CCM kimekuwa Chama cha wakulima na wafanyakazi na alama ya bendera yake ni jembe na nyundo lakini hivi sasa kuna kikundi lingine la wafanyabiashara ambapo pia kuna kundi kubwa la wamachinga na mama lishe.

“Wote hao ni wafanyabiashara, wanafanya kazi kwa kujitegemea, wanaanza kazi kwa mtaji mdogo, hivyo lazima kuwepo na mazingira yatakayowawezesha kujiendeleza kibiashara badala ya kuwekewa mlolongo wa sheria na kanuni za kodi zinazosababisha mitaji yao kumaliza hata kabla ya kuanza biashara zao.

“Kazi ya Serikali ni kuhakikisha hao wanaofanya kazi kwa kujitegemea kuwa uhuru zaidi,wasisumbuliwe”amesema Kinana alipokuwa akizungumzia umuhimu wa mazingira rafiki ya watu kujitafutia riziki zao.

Aidha Kinana amewakumbusha madiwani na wabunge wa CCM kusimama imara kwa kutoruhusu uwepo wa sheria zinazosababisha kero kwa wananchi. “Madiwani mkiona sheria zinaletwa hazina uhusiano na wananchi kataeni.

“Sheria ikiletwa kwanza ipelekeni kwa wananchi waiangalie na kisha watoe maoni yao, sheria nyingi zinatungwa na kupelekwa tu kwa wananchi, hivyo kutojua sheria inasemaje. Serikali msaidieni mwananchi aamue mambo yake yaende vizuri na apate fedha , akishakuwa na fedha za kutosha kodi atatoa bila kusumbua.

“Watu wengi wanaishi maisha ya kusaka riziki yao kwa kila siku siku ya moja, mtu anakuja anataka kodi bila kujali mfanyabiashara kauza au hajauza. Sheria ya kodi inaeleza kama biashara yako haijafika mtaji wa Sh.milioni nne hautakiwi kulipa kodi.

“Nina uhakika tukitengeza mazingira rafiki watanzania wenye kipato cha chini kufanya biashara na wakapata fedha wenyewe watalipa kodi kwa hiyari yao.Nampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza kodi ipatikane kwa busara , sio kwa vitisho,”amesema Kinana.

Aidha amesema ni vema kwa makundi mengine kwenye nyanja mbalimbali yapewe nafasi ya kufanya shughuli zao za kuleta maendeleo yao binafsi na Taifa bila kusumbuliwa huku akieleza wazi Serikali haiwezi kuajiri watu wote, hivyo kukiwa na mazingira mazuri watu watafanya kazi zao na kujiajiri.

“Huwa ninasoma magazeti utaona Serikali imetangaza ajira lakini ajira hizo ni chache ukilinganisha na mamilioni ya wasio na ajira, hivyo Serikali iifungue hii nchi vijana wapate ajira. Kwa wakulima turahisishe maisha ya wakulima , kuna haja ya kuwepo utaratibu mzuri wakulima wadogo kulisha viwanda vikubwa kwa mfano viwanda vya sukari na mkonge.”

“Chama Cha Mapinduzi ndio kimeingia mkataba na wananchi na ndio imeingia mkataba na Serikali. Wananchi wakisema hapana nasi lazima tuiambie Serikali, na kazi hii niwaahidi tutaifanya,”amesema Kinana.


Makamu Mwenyekiti CCM Bara Ndugu Abdulrahman Kinana akizungumza mbele ya wana CCM Mkoa wa Tanga kwenye kikao cha ndani akiwa wilayani Korogwe katika ukumbi wa Lembeni mjini humo, leo Jumatatu April 25,2022.PICHA NA MICHUZI JR-MMG

Mbunge wa jimbo la Korogwe Mjini Mhe. Dkt. Alfred Kimea akizungumza Mbele ya Meza Kuu na Wapiga kura wa jimbo lake waliofika kwenye ukumbi huo kumsikiliza Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndugu Abdulrahman Kinana.

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Shaka Hamdu Shaka akizungumza mbele ya wana CCM wakiwemo viongozi wa ngazi mbalimbali za Mkoa wa Tanga leo Aprili 25, 2022, katika ukumbi wa Lembeni mjini Korogwe kwenye ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndugu Abdulrahman Kinana

Makamu Mwenyekiti CCM Bara Ndugu Abdulrahman Kinana akisoma taarifa ya chama ya mkoa,kulia ni KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Shaka Hamdu Shakana kushoto ni Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Tanga Ndugu Henry Shekifu
Makamu Mwenyekiti ccm Bara comrade Abdulrahman Kinana akisalimiana na baadhi ya Wanachama nje ya ukumbi baada ya kumaliza kikao chake cha ndani akiwa wilayani Korogwe katika ukumbi wa Lembeni mjini humo, leo Jumatatu April 25,2022.
Makamu Mwenyekiti ccm Bara comrade Abdulrahman Kinana akizungmza jambo na mmoja wa Waendesha Boda boda nje ya ukumbi baada ya kumaliza kikao chake cha ndani akiwa wilayani Korogwe katika ukumbi wa Lembeni mjini humo, leo Jumatatu April 25,2022.




Makamu Mwenyekiti CCM Bara Ndugu Abdulrahman Kinana akiagana na Wana CCM mara baada ya kuzungumza nao kwenye kikao cha ndani wilayani Korogwe katika ukumbi wa Lembeni, leo Jumatatu April 25,2022.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...