Na Amiri Kilagalila,Njombe
Mkurugenzi
wa halmashauri ya mji wa Njombe Kuluthum Sadick amewaagiza wakuu wa
shule za sekondari za serikali kwenye halmashauri hiyo kuhakikisha
wanajenga misingi bora ya elimu kwa wanafunzi wao tangu wanapoingia
kidato cha kwanza ili wanapomaliza masomo yao wafaulu kiwango cha daraja
la kwanza na la pili pekee.
Agizo
hilo amelitoa wakati akikabidhi zawadi kwa walimu wa shule ya sekondari
ya Uwemba iliyopo katika halmashauri ya mji Njombe baada ya kufanikiwa
kufuta alama sifuri katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne
uliofanyika mwaka jana nchini kote.
Amesema
katika kipindi hiki ambacho yeye ni mkurugenzi wa halmashauri hiyo
hataki kuona mwanafunzi anakosa ufaulu wa daraja la kwanza na la pili
kwenye mitihani yao ya taifa katika shule zote za sekondari za
halmashauri hiyo.
Amesema
endapo wanafunzi wataelezwa na kujengewa uwezo tangu awali wanapojiunga
na kidato cha kwanza basi wataweza kufanya vizuri kwenye mitihani yao.
"Mkiwaambia
watoto toka mwanzo wanajiunga kidato cha kwanza mpaka kufikia kidato
cha watakuwa wamezoea kuwa shule inayotakiwa ni ufaulu wa daraja la
kwanza na la pili"alisema Kuluthum.
Aliwapongeza
walimu wa shule hiyo kwa kuhakikisha wanafuta ufaulu wa alama sifuri
katika mtihani wa kidato cha nne mwaka na kuwataka kuweka nguvu zaidi
ili kufuta ufaulu wa daraja la nne na la tatu.
Afisa
elimu taaluma sekondari wa halmashauri ya mji wa Njombe Huruma Chaula
alisema shule ya sekondari Uwemba ni miongoni mwa shule mbili za
serikali zilizopo kwenye halmashauri hiyo ambazo zimefanikiwa kufuta
sifuri kwenye matokeo ya kidato cha nne katika mtihani wa mwaka jana.
Alisema
shule nyingine iliyofanikiwa kufuta alama sifuri kwenye mtihani wa
kidato cha nne katika halmashauri hiyo ni shule ya sekondari Matola
ambayo pia ni serikali.
Alisema
kuna mkakati uliowekwa na halmashauri hiyo wa kuhakikisha kila shule
inakuwa na wanafunzi wasiopungua watano ambao wanafaulu kwa daraja la
kwanza kwenye mtihani wa taifa wa kidato cha nne ambapo shule ya
sekondari Uwemba imefanikiwa katika hilo.
"Matokeo
haya na hafla hii imeandaliwa makusudi na sisi kama idara tumeipokea
kwasababu imekidhi vigezo kwa isingekuwa hivyo hata sisi tusingekuja
hapa" alisema Huruma.
Mkuu
wa shule ya sekondari Uwemba Alex Chengula alisema wanafunzi wa kidato
cha nne ambao walihitimu masomo yao hapo mwaka jana walikuwa 162 huku
wavulana wakiwa 70 na wasichana 92.
Amesema
matokeo ya wanafunzi hao kwenye mtihani huo daraja la kwanza walikuwa
wanafunzi 5, daraja la pili wanafunzi 13, daraja la tatu 28 na daraja la
nne wanafunzi 116.
Amesema
katika matokeo ya kidato cha sita kwa mtihani wa taifa hapo mwaka jana
daraja la kwanza walikuwa wanafunzi 43, daraja la pili 63, daraja la
tatu 12 na hakukuwa na wanafunzi waliopata daraja la nne.
"Tumepanga
mikakati mbalimbali ambayo itatufanya tuendelee kufanya vizuri zaidi ya
matokeo haya ambayo tunapongezana leo na mikakati hiyo ni kutoa
mitihani mingi iwezekanavyo katika madarasa ya mitihani ya taifa kwa
kufuata muundo wa baraza la mitihani la taifa" alisema Chengula.
Diwani
wa kata ya Uwemba Jactan Mtewele aliwashukuru walimu wa shule hiyo
pamoja na wazazi wa wanafunzi kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha
wanatokomeza ufaulu wa daraja sifuri kwenye shule hiyo.
Aliwataka
wanafunzi,wazazi na walimu kuendelea kujenga mahusiano mazuri ili shule
hiyo iendelee fanya vizuri katika mitihani ya taifa.
" Tumejitahidi sana kuwa na mahusiano mazuri ndiyo maana leo tumefika hapa lakini pia jambo lingine ni uwepo wa nidhamu baina yetu sote" alisema Mtewele
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...