Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imeahidi kutenga fedha nyingi kwaajili ya kuwapa miradi ya ujenzi makandarasi wazalendo ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo kutekeleza miradi mikubwa huku ikiwataka wawe waaminifu.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa, wakati akifungua mkutano wa mashauriano kwa makandarasi wa ndani unaoendelea mkoani Dodoma.

Mkutano huo wa siku mbili ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), unaofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikweye Convention Center unawakutanisha makandarasi, wahandisi, wasanifu majenzi, waajiri na watunga sera kutoka serikalini.

“Nitamuomba Rais Samia suluhu Hassan atoe fedha kwa miradi mikubwa itakayotekelezwa lakini mkipewa kazi naomba muwe na bei halisi ambazo hazitatutisha na tunataka kuona thamani ya fedha ili tuone umuhimu wa kuwapa miradi,” amesema

Waziri Mbarawa amesema makandarasi wanawajibu wa kuinua uchumi wa nchi hivyo wanapaswa kutambua jukumu hilo wanapopewa miradi kwani wakichelewesha au kufanya chini ya kiwango wanakwamisha maendeleo ya nchi na kuwakosesha wananchi haki ya kutumia miradi hiyo kwa wakati.

Amesema serikali inafikiria upya utaratibu wa kujenga miradi kwa kutumia watalamu wake yaani Force Account ili kuanza kuwatumia makandarasi wazalendo kama sehemu ya kuwainua kiuchumi na kitalamu

“CRB mmezungumzia Force account sasa nawaagiza tumieni wataalamu wenu kufanya utafiti kama sababu zilizoifanya serikali kutumia utaratibu huo zipo au hazipo, serikali ya awamu ya sita ni sikivu na kama hakuna haja ya kutumia utaratibu huo tutawapa kazi nyingi ila muwe waaminifu,” amesema

Amesema baadhi ya makandarasi wazawa wamekuwa wakichelewesha miradi kwa miaka mingi hali ambayo imekuwa ikiikatisha tamaa serikali kuwapa miradi na aliishukuru Bodi ya CRB kwa kuwapa mafunzo ya kuwajengea uwezo mara kwa mara.

“Nenda maeneo kama Musoma useme unataka kuwapa kazi ya ujenzi wa barabara makandarasi wazawa usikie watakavyopiga kelele na nawaambia bora ukataliwe na serikali kuliko wananchi maana watakupiga mawe,” amesema

Waziri Mbarawa alisema serikali ya awamu ya sita imekuwa ikiwalipa makandarasi kila wanapowasilisha vyeti vya kukamilisha kazi na itaendelea kufanya hivyo ili kuwawezesha kufanyakazi kwa ufanisi na kumaliza kwa wakati.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Consolata Ngimbwa ameiomba serikali kuachana na utaratibu wa Force Account na kuwapa makandarasi wa ndani kufanya miradi hiyo kwani wengi wao kwa kukosa kazi wako kwenye hali mbaya.

Amesema makandarasi wa fani ya ujenzi waliosajiliwa na bodi wako zaidi ya 4,000 na wamiliki wake wameathirika wao na wategemezi wao kwa kiwango kikubwa kutokana na kukosa kazi kwa muda mrefu na wengine wameshakata tamaa.

“Mheshimiwa Waziri tunaomba serikali izisaidie hizi kampuni maana hawa wamiliki wanawategemezi wao na CRB imejitahidi kuwapa mafunzo mara kwa mara na kwa kweli wengi wamebadilika na mkiwapa kazi tuna uhakika watafanya vizuri sana,” amesema

“Serikali iliamua kufanya yenyewe kazi baada ya kuonekana bei zetu siyo halisia na hatukamilishi miradi kwa wakati lakini baada ya mafunzo ambayo CRB imeyafanya kwa miaka mitatu wamebadilika kabisa tunaomba muwape kazi,” amesema

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kufungua mkutano wa mashauriano kwa makandarasi wazalendo jijini Dodoma
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akimpa cheti mmoja wa wadhamini wa mkutano wa mashauriano kwa makandarasi ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), jijini Dodoma jana . Kushoto ni Mwenyekiti wa CRB, Consolata Ngimbwa
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Wizara  na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), alipowasili jana kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention kufungua mkutano wa makandarasi wazalendo jana mkoani Dodoma ulioandaliwa na (CRB)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...