Diwani wa Kata ya Unyambwa, Shabani Magwe (katikati) akishukuru Serikali baada ya kupokea mabomba hayo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WANANCHI wa Manispaa ya Singida wataondokana na kero ya maji kufuatia
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) kuanza kutekeleza mradi wa maji wenye thamani
ya Sh.540 Milioni katika Manispaa hiyo.
Mhandisi wa Ufundi wa SUWASA Mkoa wa Singida, Richard Kasase, aliyasema hayo
wakati wa uanzaji wa uchimbaji wa kisima cha maji cha mradi wa Kata ya Mwankoko ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu
wa Wlaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri ambaye alikwenda kujionea uchimbaji wa kisima hicho ambacho kinachimbwa kwa fedha UVIKO-19.
Alisema mradi huo utakapo kamilika utaongeza kiwango cha upatikanaji wa
maji katika manispaa hiyo kutoka lita za ujazo milioni 10 hadi kufikia lita milioni 12 kwa siku.
"Mahitaji ya maji kwa manispaa ni lita 14 milioni kwa hiyo pamoja na
ongezeko hilo litafanya upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85.7 kutoka asilimia 71.4 ya sasa," alisema Kasase.
Kasase alisema mradi huo
unatekelezwa kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na
mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Alisema mbali ya mradi huo upo mwingine utakaoanza katika mwaka wa fedha wa
2022-/2023 wenye thamani ya Sh.Bilioni 1, mwingine ni wa
uboreshaji wa huduma ya maji wa miji 28 wa fedha za mkopo wa masharti nafuu
kupitia benki ya India ambao ni mkubwa sana na utaongeza visima nane na kuwa unatakribani kilometa 385.
Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA Mkoa wa Singida Sebastian
Warioba akipokea mabomba ya mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji Kata ya Unyambwa alisema mabomba hayo
yatalazwa kwenye eneo lenye urefu wakilometa 3.8.
Aliongeza kuwa mabomba hayo yenye kipenyo cha inchi tatu yana thamani ya
Sh.83 Milioni na kuwa ni sehemu ya mradi wa maji wa Unyambwa ambao ukikamilika utamaliza kazi ya kuwapatia maji wananchi na kuwa
fedha hizo zimetoka kwenye Mfuko wa Taifa wa Maji ambapo katika mwaka huu wa
fedha unaokwisha SUWASAilikuwa imetengewa Sh.200 Milioni na mabomba hayo ni sehemu ya kiasi hicho cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya Manispaa hiyo.
Warioba alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa
fedha hizo ambazo zimewawezesha kuendelea kutoa huduma ya kuwafikishia maji
wananchi wa Manispaa ya Singida.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya N & Ground Water
Tanzania LTD ya Dodoma iliyopewa zabuni ya kuchimba kisima kimoja cha mradi
huo eneo la Mwankoko, Mhandisi Naftal Mandi aliishauri serikali akisema
kuwa miradi hiyo inakuwa na upotevu mkubwa
wa fedha hivyo eneo ambalo linakwenda kufanyika kwa mradi husika linatakiwa
usanifu wa kitaalam kwa kuchimba shimo dogo ambalo gharama yake itakuwa ya
chini na baada ya kupata matokeo na kubaini kuwepo kwa maji ndipo kazi hiyo
inapaswa kuendelea.
“Kwa namna hiyo itasaidia badala ya kuanza kuchimba tu bila ya kufanya
usanifu huo ambapo mara nyingi baada ya kufanyika kwa kazi hiyo bila kufanya
usanifu huo wanajikuta wametumia fedha nyingi na maji yanakuwa hayapo hivyo
Serikali kuingia hasara” alisema Mandi.
Mandi aliishauri Serikali kuwatumia wakandarasi wenye uzoefu wa kutosha
kwani sio kila mkandarasi anauwezo wa kufanya kazi hiyo hivyo aliomba wawatumie
wakandarasi waliosajiliwa na wizara na kutambulika na jambo hilo likifanyika
litasaidia kuokoa fedha nyingi za Serikali zinazopotea kwa kutumia wakandarasi
wasio na uzoefu wa kazi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri alisema ili upatikanaji wa maji uongezeke kwa wananchi Serikali imetenga fedha za kuhakikisha kila mkoa unapata mitambo ya kuchimba mabwawa na bado wizara itakuwa na mitambo mingine ya kuchimba visima vya namna hiyo na kuwa zoezi hilo la uchimbaji wa visima litakuwa endelevu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...