Na Thobias Mwanakatwe, Ikungi
WAKULIMA wa kata saba zinazolima viazi vitamu wilayani Ikungi mkoani
Singida wamelalamikia kukithiri kwa vitendo vya wafanyabiashara na madalali
kununua mazao yao kwa kutumia vipimo vya lumbesa visivyokubalika kisheria.
Malalamiko hayo yalitolewa juzi na viongozi wa kata ya Puma wakati Mkuu wa
Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro, alipofanya mkutano na madiwani, wenyeviti wa
vijiji, vitongoji, watendaji na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili
ya kusikiliza kero zinazowakabili wananchi kwenye maeneo yao.
Kata zinazolima viazi katika Wilaya ya Ikungi ni Puma, Kituntu, Ihanja,
Isyeke,Makiungo, Dung'unyi na Ikungi.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ( UVCCM) kata ya Puma,
Hangida Ramadhani, alisema wafanyabiashara hao wamekuwa wakienda katika maeneo
ya vijiji vya kata hizo na kutaka kuuziwa viazi kwenye magunia yaliyojazwa
kupita uzito wa kawaida wa kilo 100.
Ramadhani alisema kwa ujazo wa lumbesa wakulima wamekuwa wakiuza viazi kwa
bei ya Sh.55,000 kwa ujazo wa zaidi ya kilo 200 badala ya kilo 100 unaokubalika
kisheria.
Alisema kuwa ni vyema Serikali ikaingilia kati tatizo hilo ili
wafanyabiashara hao wasiendelee kuwanyonya wakulima wakati wanaponunua mazao na
hivyo kuendelea kuwa masikini.
Alisema ununuzi wa mazao hayo kwa kutumia vipimo hivyo hauwanufaishi
wakulima ambao wamekuwa wakitumia nguvu kubwa na muda mrefu katika kuzalisha,
badala yake huwapa faida wafanyabiashara.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro, akijibu malalamiko hayo alisema
serikali itashughulikia tatizo hilo na kwamba imeshaanza kwa zao la alizeti
ambalo nalo kulikuwa na ulaghai kama huo kwa wakulima.
Muro alisema changamoto kubwa iliyopo ni kwa wakulima wenyewe ambao baadhi
yao wamekuwa wakikubaliana na kuwauzia wafanyabiashara mazao yao kwa bei ya
chini yakiwa bado yapo shambani kwa vipimo vya lumbesa ambavyo kimsingi
havikubaliki.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...