Na Mashaka Mhando, Korogwe
BENKI ya National Microfinance (NMB) tawi la Korogwe limewafunda wananchi wa jimbo la Korogwe Vijijini namna ya kuweza kupata mikopo itokanayo na benki hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya meneja wa tawi hilo, Ofisa Mikopo wa tawi hilo Sara Lema, aliwaomba wananchi ili waweze kupata mikopo ni vema wakafika katika tawi la benki hilo, wakafungua akaunti ya akiba.
Ofisa huyo alikuwa akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyoandaliwa na mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini Timotheo Mnzava anayeendelea kukagua na kuhamasisha Maendeleo ya jimbo lake.
Alisema wafike katika tawi hilo kufungua akaunti za vikundi kwa vijana, akina mama na walemavu ambapo alitoa ofa kwa vikundi vitatu atawasajilia bure.
"Ndugu zangu wa Makumba, nawaomba mje mfungue akaunti zenu katika tawi letu la benki lililopo pale Korogwe mjini, vikundi vitatu nitavisajili bure ikiwemo Mtoto akaunti tano," alisema. Sarah.
Ofisa huyo alisema kuwa pia benki hiyo inatoa mikopo kwa ajili ya wakulima na wafugaji, mikopo ya wafanyabiashara ambayo hutolewa pindi kikundi kitakapokua na akaunti.
Alisema pia wanatoa mikopo ya pensheni kwa ajili ya wafanyakazi waliostaafu, mikopo ya walimu, madaktari, maofisa kilimo pamoja na maofisa wengine waliopo katika ngazi za vijiji na kata.
"Wananchi msiogope fikeni kwenye tawi letu mpate maelekezo ya namna ya kukopa, mfano unaweza kukopa pikipiki kwa ajili ya bodaboda, guta, bajaji na hata trekta kwa ajili ya kilimo," alisema Sarah.
Kuhusu huduma zinazotolewa na benki hiyo, ofisa huyo alisema kwasasa wamewasogezea huduma kupitia mawakala wao waliopo katika maeneo ya Kulasi, Magoma na hivi karibuni watafungua ofisi ya uwakala katika kijiji cha Mashewa.
Alisma mawakala hao wanahusika na ulipaji wa miamala ya serikali, utoaji wa fedha na shunguli nyingine nyingi za kibenki.
Sarah Lema ofisa mikopo wa benki ya NMB tawi la Korogwe akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kitivo Korogwe
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...