Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwamba baada ya Chama hicho kuridhia mchakato wa Katiba mpya kukufuliwa upya kazi iliyobakia ni Serikali kuona namna nzuri ambayo itafanikisha mchakato huo kwa kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kutosha kushiriki.
Akizungumza leo Julai 12,2022 Mjini Zanzibar alipokuwa kwenye kituo cha redio Zenj FM Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka amefafanua upatikanaji wa Katiba mpya Chama hicho hakiwezi kuipangia Serikali.
Amesema CCM imetoa wazo kutaka mchakato wa Katiba mpya ufufuliwe na uendelee, hivyo Serikali ndio watakuja na kuwaambia wamejipangaje kuufanikisha kwasababu Katiba sio ya wanasiasa bali Katiba ni ya wananchi.
“Kwa hiyo wao(Serikali) wakishaweka mazingira mazuri ya kuona namna njema ya kutushirikisha sisi ili kusaidiana mawazo ya pamoja nadhani muelekeo kama ni mwaka huu au ni mwakani watatueleza.
“Lakini hakuna udharura , lazima tukubaliane hakuna udharura tuende taratibu lakini kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe. Kuna mtu aliwahi kuniuliza mnawashirikisha wananchi vipi wakati na wenyewe wameshatoa maoni. Ndo wametoa lakini kutoa maoni ni jambo moja.
“Kwa mfano leo hii tuseme tunakwenda kufanya maamuzi ya Katiba iliyopendekezwa mwananchi wa Makunduchi anafahamu kilichopendekezwa ndani ya hiyo Katiba?Mmwananchi Nungwi anafahamu kilichopendekezwa?Je mwananchi wa Pujini anafahamu?
“Kwa hiyo lazima tuweke msingi wa kutengeneza mazingira rafiki ya elimu ya uraia ili kuwaambia Watanzania maamuzi mnayokwenda kufanya ni haya , kwasababu maamuzi haya tayakwenda kuishi miaka 50 mbele,”amesema Shaka.
Ameongeza wote wamekuwa mashahidi katiba iliyopo hivi sasa imefanyiwa marekebisho mara 14 tokea mwaka 1977 mpaka leo.
“Hivyo leo tukisema tena inafanyiwa marekebisho, tukisema tunaandika Katiba mpya bila ya ushiriki wa wananchi kwa asilimia 100 nadhani hata na wao hawatuwatendeki haki.
“Hivyo tusijipe nafasi wanasiasa tukajifanya ndio tumehodhi ajenda hii, ajenda hii ni ya wananchi na Serikali naamini kwenye hili italiangalia vizuri na itakuja na utaratibu ambao tutashiriki wanasiasa , na watashiriki wananchi, hivyo tuwende taratibu.”








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...