Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufungamanisha sekta za kilimo na nishati kupitia mikakati mbalimbali ya kukuza uchumi inayotekelezwa kwenye nchi hizo.
Akizungumza leo katika Mkutano Mkuu wa 51 wa Jukwaa la Mabunge ya SADC, unaoendelea Jijini Lilongwe nchini Malawi, Dkt. Tulia amebainisha umuhimu wa kufungamanisha sekta hizo ili ziwezeshe ukuaji wa uchumi katika ukanda wa SADC.
“Endapo tunahitaji nchi zetu ziweze kujitegemea kwenye suala la usalama wa chakula, tunapaswa kujifunza kupitia nchi zingine zilizofanikiwa katika sekta hii kama zilivyoainishwa kwenye taarifa ya kamati ya Chakula.”
“Tunapaswa kuweka kipaumbele kwenye miundombinu wezeshi itakayosaidia kukuza sekta ya kilimo, kama ni sekta ya nishati basi twende pamoja kama Jumuiya kuhakikisha inakuza kilimo chetu,” amesema.
Akitolea mfano nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Spika amesema “Nakubaliana na wenzetu wa Kongo kuwa mradi wa umeme wa maji wa Inga unaweza kutoa umeme kwa nchi zote za SADCna hivyo kusaidia katika juhudi za kukuza sekta ya kilimo.”
Dkt. Tulia amewaomba wajumbe wa Mkutano huo kuweka nguvu kwenye maeneo mengine ya kiuchumi yatakayofungamanishwa ili kukuza sekta ya kilimo kabla ya kufikiria kupata wawekezaji wakubwa watakaokuja kuwekeza katika sekta hiyo.
Aidha, Dkt. Tulia ametoa wito kwa wajumbe hao kuzishauri nchi zao kuondoa vikwazo katika biashara ya mazao mbalimbali yanayozalishwa kwa wingi miongoni mwa nchi hizo kama sehemu ya juhudi za kukuza sekta ya kilimo.
Kadhalika, Mhe.Spika ameshauri kuimarishwa kwa ushirikiano wa biashara baina ya nchi hizo ili kuhakikisha kunakuwapo na soko la uhakika kwa mazao yanayozalishwa na wakulima.
“Iwapo nchi mojawapo katika ukanda huu inazalisha kwa wingi zao fulani, kwanini nchi zingine wanachama zisiiunge mkono kwa kununua zao hilo badala ya kwenda kununua katika nchi zilizo nje ya Jumuiya ya SADC,kwa kufanya hivyo tutatengeneza soko la ndani la bidhaa za kilimo,”amesema.
Awali, Mjumbe wa Jukwaa hilo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya SADC PF ya Chakula, Kilimo na Maliasili, Mhe.Ishmael Onani amewasilisha Taarifa ya Kamati hiyo iliyobeba Kaulimbiu ya Ushiriki wa Mabunge katika ujenzi wa mifumo imara ya kilimo kupitia usimamizi wa fedha za umma.
Amesema, pamoja na ukweli kwamba kilimo ni kati ya sekta muhimu za kukuza uchumi na kupunguza umaskini lakini kumekuwa na uwekezaji mdogo kwenye sekta hiyo jambo linalosababisha ukuaji hafifu wa uchumi kwa nchi za SADC.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...