Na Victor Masangu,Pwani
Mamlaka
ya maji safi na usafi wa mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika
kukabiliana na changamoto za ukosefu wa maji imeaanza kuweka mipango
madhubuti na kuchukua hatua stahiki wakati wa ukame unapotokea kwa
kujenga mabwawa mbali mbali kwa ajili ya kutunzia maji.
Kauli
hiyo imetolewa na mtendaji mkuu wa mamlaka ya maji safi na usafi wa
mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja ambapo
alisema kwamba Ujenzi wa mabwawa hayo yataweza kusaidia wananchi
kuondokana na adha na kero waliyokuwa wakiipata.
Kuhemeja
alifafanua kuwa kiwango kilichopo kwa sasa cha upatikanaji wa maji
kitaweza kutuvusha katika kipindi kizima cha kiangazi na kwamba wananchi
wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wasiwe na shaka yoyote.
Pia
Luhemeja katika hatua nyingine amewataka wananchi wote kuhakikisha
kwamba wanatunza na kulinda vyanzo vyote vya maji ili kuwepo na
upatikanaji wa maji ya uhakika katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Dar
es Salaam pamoja na Mkoa wa Pwani.
“Itakumbukwa
kwamba mnamo mwaka jana maeneo kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam
yalikumbwa na tatizo la uhaba wa maji nah ii ni kutokana na ukame
uliosababishwa na kutokunyesha kwa mvua za vuli na ndio maana wakuu wa
mikoa hii miwili wameweza kuungana kwa pamoja na kamati za ulinzi na
usalama wakaona ni jambo la busara kuweza kutembelea na kujionea vyanzo
vya maji,” alisema Luhemeja.
Kadhalika
Luhemeja alisema kwamba mamlaka hiyo kwa sasa imeweka mipango madhubuti
kwa ajili ya kuweza kuendelea kufanyabjitihada za makusudi za
kuhakikisha kwamba kiasi cha maji kilichopo kwa sasa kinalindwa ili
kuweza kudhibiti hali ya upotevu wa maji.
Kadhalika
aliziomba kamati za ulinzi na usalama za mikoa yote miwili kushirikiana
kwa dhati ili kuweza kuwadhibiti baadhi ya watu ambao wamekuwa
wakiyachepusha maji na kwamba ana imani kubwa bwawa ambalo wamelijenga
kwa ajili ya kuhifadhia maji litakuwa ni mkombozi hasa katika kipindi
chote cha ukame.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amosi Makala ametoa wito kwa
wananchi pamoja na viongozi mbali mbali wa dini zote kuhakikisha
wanafanya maombi kwa ajili ya kuombea mvua za vuli zinyeshe ili kusiweze
kutokea tena majanga ya ukame kama ilivyoweza kutokea katika kipindi
cha mwaka jana hali ambayo ilipelekea vyanzo vya maji kupungua na
kusababisha wananchi kupata usumbufu.
Pia
katika ziara hiyo Makala ameridhishwa na kazi amabzo zinafanywa na
viongozi wa Dawasa na kuwahakikishia wakazi wa Mkoa huo kuwa hali ya
upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa sasa ni nzuri hivyo
wasiwe na shaka.
“Ndugu
zangu waandishi wa habari mwaka jana kuliweza kutokea hali ya ukame wa
maji kutokana na kutonyesha kwa mvua za vuli lakini nataka niwaambia
kitu kikubwa ni kuomba Dua na maombi mvua zinyeshe na sio kuilaumu
serikali kwani serikali haileti mvua na kwamba tutazidi kushirikiana na
mamlaka husika lengo ikiwa hali ya maji iweze kupatikana katika kipindi
chote,”alisema Makala.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amekemea tabia ya baadhi ya
wananchi wenye tabia ya kuchepusha maji kutoka kwenye vyanzo vya maji na
kuahidi kuwachukulia hatua kali kwa wale wote ambao watahusika kwani
lengo la serikali ni kuwapelekea huduma ya maji safi na salama katika
maeneo mbali mbali.
“Kitu
kikubwa ninachowaomba wanachi kuhakikisha kwamba wanaachana mara moja
na tabia ya kuchepusha maji katika vyanzo vya mto ruvu kwani
wakifanya hivyo kunapelekea maji yapungue katika vyanzo vyetu vya
maji”alisema Kunenge.
Ujio
wa ziara hiyo ya siku moja ambayo imefanywa na wakuu wa mikoa ya Dar es
Salaam na Pwani pamoja na wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama wa
mikoa miwili imeweza kusaidia kujionea chanzo cha maji Cha mto Ruvu
pamoja na mitambo ya Ruvu juu na Ruvu chini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...