Na. Catherine Mbena/TARANGIRE

Kamati ya Kudumu ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongeza juhudi zinazofanywa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), katika kuhakikisha miradi ya uboreshaji miundombinu inafanyika kwa ubora na kwa wakati walipotembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire leo kukagua miradi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Daniel Sillo (MB) alisema “Niwapongeze TANAPA chini ya Wizara Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi hii pamoja na maboresho mnayoyafanya kwani maboresho haya yatakuza uchumi wa taifa letu na tunaamini mkiboresha miundombinu yote italeta tija kwa uchumi wa Taifa.”

Pia, Mhe.Sillo aliwaasa watendaji wote wa TANAPA kuendelea kusimamia miradi yote kwa uadilifu na kila mmoja atimize wajibu wake.

Akitoa wasilisho fupi kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA, William Mwakilema, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Uendelezaji wa Hifadhi za Taifa, Paul Banga alisema zaidi shillingi billioni 46 zilitengwa kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ambapo Hifadhi ya Taifa Tarangire ilipata 2.7 bilioni ikiwa ni kwa ajili ya kuboresha viwanja vya ndege na matengenezo ya barabara na vivuko.

Miradi mingine inayotekelezwa na fedha hizi ni pamoja na ujenzi wa madaraja na vivuko, ukarabati wa viwanja vya ndege, ujenzi wa barabara na njia za kupanda milima, eneo la kutua helikopta za uokozi, ujenzi wa malango ya ukusanyaji mapato, ununuzi wa mitambo na magari pamoja na ufungaji wa mifumo ya ufuatiliaji wa magari na mitambo.

Akitoa shukrani kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Jenerali (mstaafu), George Waitara alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kutoa pesa hizi za Mradi wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19 ili kuinua sekta ya utalii.

“Namshukuru sana Mhe. Rais kwa kuamua kutoa pesa hizi za mradi wa mapambano dhidi ya UVIKO - 19. Tulifika mahali tukakwama kabisa kwani hii UVIKO – 19 ilikuwa pigo sana kwa Uhifadhi na Utalii.” Alisema Waitara

Aidha, Waitara aliongeza kuwa Kukamilika kwa miradi ya miundombinu kutawezesha watalii kufanya safari zao kwa usalama, na ndani ya wakati hivyo kuona thamani ya fedha zao.

Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (MB) aliwaahidi wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti kuwa miradi yote inayotekelezwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inakamilika ndani ya muda uliopangwa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imemaliza ziara yake ya kukagua miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Tarangire leo na itaendelea na ziara hii katika Hifadhi za Taifa Mkomazi na Kilimanjaro.



















 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...