Na Raphael Kilapilo
Wananchi kata ya Mpuguso wilayani Rungwe, Mbeya wameipongeza Serikali kwa kuwajali baada ya kukamilika kwa barabara za Masebe-Bugoba-Lutete (KM 7.2) na Barabara ya Masabe DSP-Mpuguso TTC-Bugoba Kibaoni (KM5.0), zilizojengwa kwa kiwango cha lami.
Pongezi hizo zimetolewa na wananchi hao wakati wa ziara ya Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoani Mbeya; wakikagua Mradi wa barabara za “Agri-Connect”, wenye lengo la kuboresha miundombinu ya barabara maeneo yanayolimwa mazao ya biashara.
Akizungumza na wajumbe wa bodi diwani wa Kata ya Mpuguso Mhe. Japhet Kagugu alisema kuwa anaishukuru sana Serikali kwa ujenzi wa barabara hizo za lami ambazo zimeleta ukombozi na manufaa makubwa kwa vijiji vyote vinavyopitiwa na barabara hizo katika kata za Mpuguso, Isonda na Ilima.
“Kiuchumi barabara hizi zimetuletea manufaa makubwa katika kusafirisha mazao yetu ya chai, kahawa, ngano, Ndizi, viazi na parachichi. Kabla ya barabara hizi mazao yalikuwa yanaharibika kutokana na ubovu wa barabara, lakini kwa sasa mazao yanafika sokoni kwa uhakika na imesaidia kukuza kipato cha mwananch mmoja mmoja na pia Serikali imeongeza mapato,” alisema Mhe. Kagugu.
Aidha alieleza kuwa thamani ya maeneo yao imepanda na hata wageni wanakuja kununua viwanja kutokana na kuboreshwa kwa barabara.
Naye Ndugu Weston Ambakisye mkazi wa kitongoji cha Lusungo alieleza kuwa walikuwa wakiteseka sana wakati wa mvua kutokana na matope mengi na kushindwa kusafirisha mazao yao, tofauti na sasa ambapo barabara imewanufaisha sana na wanaishukuru sana TARURA kwa ujenzi wa barabara za lami.
Kwa upande wake ndugu Stiven Kayombo, mkazi wa Mpuguso alieleza kuwa kutokana na ubovu wa barabara uliokuwepo awali, walikuwa wanatumia gharama kubwa kusafirisha mazao yao na kupata hasara kubwa tofauti na sasa ambapo barabara ya lami imewakomboa.
“Mazao tulikuwa tukiuza kwa hasara kubwa mnunuzi kuja huku ilikuwa ni shida na akija alikuwa ananunua mazao kwa bei ya chini sana na si hivyo tu huduma za kijamiii kama kwenda hospitali ilikuwa ni shida. Lakini sasa tunaishukuru sana Serikali, imetukomboa na uchumi wetu umeimarika,” alisema Kayombo.
Maria Kasege mkazi wa Mpuguso alishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwajengea barabara na kuwaletea maendeleo.
“Kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kazi anayofanya, mmetutua mzigo kichwani, tulikuwa tunateseka sana , mtu alikuwa anatoka huko mashambani na mzigo kichwani hadi sokoni. Sasa tunamshukuru Mungu kwa barabara hizi hata pikipiki zinatusaidia kubeba na mazao yanafika kwa wakati,” alisema Maria.
Pia Subira Kajinga mkazi wa Mpuguso alisema kuwa walikuwa wanapata ajali nyingi kutokana na utelezi mwingi barabarani mvua zinaponyesha kabla ya barabara kujengwa. “ Sasa hatuna tatizo maisha yetu ni mazuri barabara hizi zimetuletea manufaa makubwa, tunamshukuru sana Rais wetu Mama Samia kwa kutujali.
Bodi ya Ushauri TARURA inaendelea na ziara ya kikazi mkoani Mbeya kukagua miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na iliyo kamilika ili kuhakikisha adhma ya Serikali ya kuboresha barabara za Vijijini na Mijini inatimia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...