Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Tamasha la Kwanza
la Kitaifa la Utamaduni kwenye Uwanaja wa Uhuru, Temeke mkoani Dar es
salaam,

Wasanii
kutoka Mkoa wa Mwanza wakicheza ngoma ya nyoka katika Tamasha la Kwanza
la Kitaifa la Utamaduni lililofunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
kwenye uwanja wa Uhuru, Temeke jijini Dar es slaam

Baadhi
ya washiriki wa Tamasha la Kwanza la Kitaifa la Utamaduni wakimsikiliza
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua tamasha hilo kwenye
uwanja wa Uhuru, Temeke mkoani Dar es salaam.

Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed
Mchengerwa (katikati) wakifurahia ngoma wakati Waziri Mkuu alipofungua
Tamasha la Kwanza la Utamaduni kwenye Uwanja wa Uhuru, Temeke Mkoani Dar
es salaam, Julai 2, 2022. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya
Utamaduni, Sanaa na Michewzo, Dkt. Hassan Abbas.

Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Fatuma Mtanda (wa
pili kushoto) wakati alipotembelea banda la Mkoa wa Mtwara baada ya
kufungua Tamasha la Kwanza la Kitaifa la Utamaduni kwenye uwanja wa
Uhuru, Temeke Mkoani Dar es salaam

Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha nakala za Mwongozo wa Maadili na
Utamaduni wa Mtanzania baada ya kuuzindua katika Tamasha la Kwanza la
Kitaifa la Utamaduni lililofanyika kwenye uwanja wa Uhuru, Temeke
Mkoani Dar es salam, Julai 2, 2022. Katikati ni Waziri wa Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya
Tameke, Joketi Mwegelo. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………..
*Awataka wanaojishughulisha na vitendo vinavyokiuka misingi ya maadili waache
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amefungua Tamasha la Kwanza la Kitaifa la
Utamaduni na kuwataka watu wote wanaojihusisha na vitendo viovu
vinavyokiuka misingi ya maadili waache mara moja na badala yake waamue
kuishi kwa kuzingatia mila na desturi za Kitanzania.
“…kwa kuwa
suala zima la maadili linaanzia katika ngazi ya familia na jamii,
ninatoa wito kwa wazazi na walezi, taasisi za dini, machifu na wadau
wengine, kuendelea kukemea uovu huo na kuwafunza watoto na vijana wetu
maadili mema ili kukilinda kizazi chetu cha sasa na kijacho.”
Waziri
Mkuu amefungua tamasha hilo leo (Jumamosi, Julai 02, 2022) katika
Uwanja wa Uhuru, Temeke mkoani Dar Es Salaam. Amesisitiza kuwa kuwa
familia ni kitovu cha makuzi na malezi kwa watoto na vijana. “Familia ni
asasi ya msingi na muhimu katika mfumo wa jamii na hivyo inaweza
kuendeleza maadili, malezi na urithishaji wa utamaduni wetu wa
Kitanzania.”
Waziri Mkuu amesema walezi na wazazi wanatakiwa
wajifunze kutilia maanani malezi ya watoto kwa kutenga muda wa kukaa na
watoto na vijana na siyo kuziachia shule peke yake. “Tushirikiane na
Serikali, taasisi za dini na wadau wengine, kukemea mmomonyoko wa
maadili katika Taifa letu.”
Waziri Mkuu amewataka vijana wote wa
Kitanzania waache kuendekeza tabia ya kutumia muda mrefu kwenye
mitandao ya kijamii kwa kusoma au kuangalia mambo ambayo hayaongezi
thamani ya maisha yao na badala yake watumie muda huo kufanya kazi.
“Tutumie mitandao kutafuta maarifa yanayofaa na tujikite zaidi katika
shughuli mbalimbali za uzalishaji.”
“Kwa kuwa maadili ni chimbuko
la uzalendo na utu wetu, ninaitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na
Michezo kuongeza jitihada katika kuandaa programu za elimu kwa umma
kuhusu umuhimu wa kuheshimu na kuthamini mila na desturi zetu, pamoja na
uzalendo, ili tutengeneze kizazi kinachozingatia maadili mema.
Tusikubali kamwe kuwa watumwa wa tamaduni za kigeni.”
Amesema
jukwaa mojawapo ambalo wizara hiyo inaweza kuanza nalo ni kuandaa
mdahalo wa kitaifa kuhusu mmomonyoko wa maadili, ambapo wanaweza kupata
picha halisi ya hali ya maadili ilivyo nchini kwa sababu watakutanisha
makundi mbalimbali.
“Programu nyingine ni kuunda kablu za maadili
katika shule za msingi na sekondari. Taasisi ya Kupambana na Kuzuia
Rushwa (TAKUKURU) wana klabu ambazo zinawaelimisha wanafunzi kuhusu
mapambano dhidi ya rushwa. Kwa hiyo na nyinyi Wizara kwa Kushirikiana na
TAMISEMI igeni mfano huo mzuri.”
“Nyote mtakubaliana nami kwamba
hali ya mmomonyoko wa maadili katika Taifa letu ni mbaya sana kwa rika
zote. Mlezi wetu namba moja Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na mama mlezi wa familia anaguswa sana
jambo hili ambapo, katika hotuba zake nyingi haachi kugusia suala la
maadili.”
“Vilevile, tumeshuhudia baadhi ya vitendo viovu vingi
kama vile kuongezeka kwa vitendo vya watoto kuwauwa wazazi wao; ulawiti;
wanawake kuuwawa na waume zao; ubakaji hususani kwa watoto na
wanafunzi; watoto na vijana kutowaheshimu watu wazima hususani katika
vyombo vya usafiri na kutumia lugha zisizofaa wanapozungumza na watu
wazima; uvaaji wa mavazi yasiyo na stara hususani kwa wasichana na
wavulana na matumizi ya madawa ya kulevya.”
Akizungumzia kuhusu
umuhimu wa tamasha hilo, Waziri Mkuu amesema tamasha hilo limetokana na
agizo la Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania alilolitoa akiwa mkoani Mwanza tarehe 8 Septemba, 2021 kwenye
Tamasha la Utamaduni. “Mheshimiwa Rais alielekeza yafanyike matamasha ya
utamaduni ya namna hii nchi nzima.”
“Naiagiza Wizara ya
Utamaduni, Sanaa na Michezo, iandae mwongozo wa jinsi gani matamasha
haya yataendeshwa. Pia ninaiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
kushirikiana na wadau ambao wanaandaa matamasha ya Utamaduni. “
Pia,
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa wadau wahakikishe wanaishirikisha Wizara
ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wanapoandaa matamasha yao wahakikishe
wizara husika inafahamu. “Si vema mdau unaandaa tamasha huku wizara
yenye dhamana na utamaduni haifahamu kabisa au inafahamu dakika za
mwisho.”
Akizungumzia kuhusu vyombo vya habari, Waziri Mkuu
amesema vyombo vya habari vinatakuwa viwe walimu wema wa kuhakikisha
maadili yanazingatiwa, visiwe chanzo cha mmomonyoko wa maadili.
“Hakikisheni mnakagua kazi zenu kabla hamjazirusha hewani hususani
filamu, muziki au programu zinazotoka nje ya nchi.
Kwa upande
wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema
tamasha hilo ambalo linafanyika kwa siku tatu lilianzia jana Julai
Mosi, 2022 litamalizika kesho Julai 3, 2022, limeandaliwa mahsusi katika
wiki ya kuelekea siku ya Kiswahili Duniani ambayo kilele chake ni Julai
7, 2022.
Amesema Tamasha hilo litachagizwa na shughuli
mbalimbali zikiwemo mashindano ya ngoma za kitamaduni na vyakula vya
asili pamoja na maonesho ya bidhaa mbalimbali za kitamaduni. Kauli mbiu
ya tamasha hilo inasema “Utamaduni wetu; tujiandae kuhesabiwa, kazi
iendelee.”
Amesema moja ya matokeo tarajiwa la tamasha hilo
ambalo limeshirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ni kuwepo
kwa hamasa kubwa nchini ya kupenda, kuhifadhi, kulinda, kuendeleza mila
na desturi ambazo ndio msingi wa maadili na utambulisho wa Taifa kwa
ujumla.
Awali, Mheshimiwa Majaliwa alipokea matembezi ya
utamaduni ambayo yalihusisha wananchi kutoka katika mikoa mbalimbali ya
Tanzania ambao walipita wakiwa katika magari ya wazi huku kila mkoa
ukionesha na kucheza ngoma za utamaduni za mkoa husika.Tamasha hilo
limejumuisha matembezi ya kiutamaduni (road carnaval) katika mitaa ya
jiji la Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...