Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imesema moja ya eneo muhimu wanalolisimamia ni usimamizi na udhibiti wa kemikali, hivyo ni vema wakaendelea kutoa elimu kuhusu utumiaji sahihi wa kemikali hizo katika uwezeshaji na uwekezaji.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea viwanja vya Sabasaba Dar es Salaam, Mkemia Mkuu wa Serikali Dk.Fidelice Mafumiko amesema kauli mbiu ya Serikali kwenye maonesho hayo ni uwezeshaji katika biashara.

“Na kama ni uwezeshaji katika biashara na sisi ni Mamlaka ambayo inadhibiti uingizaji wa kemikali kama malighafi za viwanda , kwa hiyo tunafanya kila liwezalo kwa njia ya mtandao lakini na ana kwa ana kuonana na wateja ili kuwaeleza mahitaji gani yanayohitajika ili waweze kuwekeza katika kemikali.

“Na tunatambua kwamba ukiwekeza kemikali ina faida sana katika uwekezaji wa uchumi katika viwanda lakini hizo zinazoingia zikitumika isivyo huwa sio sahihi kwa hiyo kwenye kauli mbiu Tanzania ni mahali sahihi kwa uwekezaji na katika biashara basi na sisi tunasaidia kuhakikisha usalama na ubora wa kemikali zinazoingia nchini,”amesema Dk.Mafumiko.

Pia wanatoa elimu kwa wananchi na hata wanaofika katika maonesho wanapata elimu ya mahitaji gani yanahitika katika kuingiza kemikali nchini.“Sisi Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali tunafanya pia uchunguzi wa kimaabara kuhakikisha ubora wa bidhaa zinazoenda kushughulika na kemikali.

“Ujumbe wangu wangu muhimu ni kwamba wadau wote wanaopita kwenye banda letu wapate elimu sahihi kuhusu utumiaji wa kemikali kama malighafi na hasa inayoenda kutumika katika uzalishaji wa viwanda,”amesema Dk.Mafumiko.

Akizungumzia kuhusu vipimo vya vinasaba maarufu kwa jina la DNA Dk.Mafumiko amesema huduma ya DNA inapatikana katika maonesho hayo kwa kutoa elimu kwa wananchi

“Katika DNA ukitaka kujua nini ambacho unahitaji na utaratibu ukoje , kwa mfano kuna mamlaka ambazo zimeidhinishwa kisheria kutegemena na mteja anataka apime vinasaba kwa ajili ya nini kwa mfano anataka kufahamu uhusiano.

“Vinasaba kwanza ni chembechembe za asili za urithi kutoka kizazi kimoja kwenda kingine, kwa hiyo basi akija hapa atapata elimu ili apime vinasaba tunaangalia suala lake je ni suala la jinai, kimahakama , kimatibabu au kijamii.Kwa mfano unataka kufahamu uhalali wa mtoto au uhalali wa wazazi kwa mtoto,”amesema.

Amefafanua ukifika utaambiwa ili upate kipimo huji wewe moja kwa moja bali unamuona ofisa ustawi wa jamii katika eneo lako husika au Wakili aliyeandikishwa ambaye ataelezwa shida ya mhusika na ndio atapeleka maombi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kipimo chao kwa kila mtu anayechukuliwa usampuli gharama yake ni Sh.100,000.

Amesema gharama hiyo iko chini sana ukilinganisha na hali halisi ya kupima vinasaba na sababu ya kuwa chini Serikali imebeba sehemu kubwa ya gharama pamoja na kufanya uwekezaji mkubwa ndani ya mamlaka hiyo.

“Ukiangalia muda tunaotumia, dawa tunazotumia, utaalam tunaotumika na mambo mengine yanayohitajika gharama yake kwa sampuli moja ni kati ya Sh.700,000 hadi Sh. 800,000.Serikali imewekeza katika vifaaa na utaalamu ndio maana gharama zinapungua hadi kufikia Sh.100,0000.

“Gharama hiyo imedumu kwa muda mrefu inakaribia mwaka 10 sasa , kwa hiyo mwito wangu wananchi wapate maelezo sahihi kulingana na mahitaji na maelezo hayo wanaweza kuyapata katika banda hili au katika ofisi zetu zilizoko katika kila kanda”.







Matukio mbalimbali katika picha wakati maofisa wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wakiongozwa na Mkemia Mkuu wa Serikali Dk.Fidelice Mafumiko wakiendelea kuwahudumia wananchi waliofika kwenye banda lao lililopo katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea viwanja vya Sabasaba Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...