Mwanasiasa Mkongwe nchini na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga ndugu Khamis Mgeja leo tarehe 06.07.2022 amechukua fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa CCM Mkoa katika ofisi ya Katibu wa CCM mkoa wa Shinyanga.
Baada ya kuchukua fomu kwa Katibu wa CCM Mkoa ndugu Donald Magesa, Mgeja aliwaonesha waandishi wa habari fomu hizo nje ya jengo la CCM Mkoa na kuongea kwa kifupi.
Kwanza Mgeja alisema "Namshukuru Mungu leo kwa kufanikiwa kutimiza nia yangu ya kuchukua fomu ya kuomba nafasi ya uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga". Pili alisema "Nakipongeza chama changu cha CCM kwa kufungua milango kwa wanachama wake kuomba nafasi za uongozi kwa ngazi mbalimbali,kuanzia shina hadi Taifa na hii ni kuonesha ukuaji wa demokrasia ndani ya chama.
Tatu komred Mgeja alisema "Nafasi ninayoiomba, nimejipima na kuona uwezo na uzoefu mkubwa ninao na hivyo ikanisukuma kuomba nafasi hii". Aidha Mgeja aliendelea kusema "kuomba nafasi ya uongozi ni hatua moja, mengine tuviachie vikao vya chama, leo yatosha kusema tuombeane kheri na kazi iendelee.
NB: Komred Mgeja amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama, serikali na taasisi mbalimbali. Amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga, Mjumbe wa Kamati ya utekelezaji UVCCM Taifa, Mjumbe wa balaza Kuu la UVCCM TAIFA, Diwani na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kahama.
Mgeja pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha mpira Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA), Mjumbe wa mkutano Mkuu wa TFF Taifa,Makamu Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU).
Kwa hivi sasa Mgeja ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation ambayo inajishughulisha na maswala ya Haki, Demokrasia na Utawala bora. Aidha Mgeja ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya waislamu Mkoa wa Shinyanga- BAKWATA.
Kichama, komred Mgeja ni Mjumbe wa Shina la CCM namba 2 pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Tawi la CCM la Nyanhembe wilaya ya Kahama 2022 hadi 2027.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...