Na Said Mwishehe, Zanzibar
KATIBU
wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Shaka Hamdu Shaka
amesema Chama hicho hakijawahi kuogopa mfumo wowote wa kimageuzi iwe
katika siasa, kiuchumi au kijamii.
Ametoa kauli hiyo leo wakati
akizungumza kwenye Kituo cha Redio cha Zenj FM Mjini Zanzibar ambapo
alifika kwenye kituo hicho ikiwa sehemu ya kutembelea vyombo mbalimbali
vya habari vilivyopo visiwani hapa baada ya kufanya ziara kama hizo
Tanzania Bara.
Akiwa katika kituo hicho cha redio pamoja na
kuelezea sababu za kufanya ziara hiyo, mmoja ya watangazaji alitaka
kufahamu iwapo CCM ina hofu yoyote wa kimageuzi iwapo mchakato wa Katiba
mpya utafanyika na kupatikana.
Akijibu swali hilo, Shaka
ameeleza Chama Cha Mapinduzi hakijawahi kuogopa mfumo wowote wa
kimageuzi na hawaogopi kwasababu wanajiamiani kwani mpaka leo bado
wamekubaki kuwa ndio tegemeo la Watanzania.
“Na hivyo vya ambavyo
mnavizungumza sisi ndio ambao tunafanya kazi ya kuvilea na tunafanya
kazi hiyo ili viweze kutukurupusha kidogo na viweze kuishi na kama
isingekuwa malezi mazuri ya CCM basi leo kwenye ramani ya vyama vya
siasa visingekuwepo.
“Kikubwa ambacho nataka kuhimiza hapa ni
uvumilivu wa kisiasa , umoja na mshikamano. Nilitegemea mngeuliza kuhusu
maridhiano ambayo tunakwenda nayo,”amesema Shaka.
Akielezea
kuhusu maridhiano amesema wanakwenda vizuri na tangu Rais wa Jamhuri ya
Muungano na Mwenyekiti wa CCM Taifa Samia Suluhu Hassan baada ya
kuingia madarakani alikutana na makundi mbalimbali.
Shaka amesema
miongoni mwa makundi ambayo amekutana nayo ni pamoja na kundi la
wanasiasa ambalo ndilo limekuja kuibua maridhiano ya kisiasa , hivyo
alikutana na a na viongozi wa Chadema , ACT Wazalendo, CUF.
“Na
atakutana na viongozi wa vyama vingine vyote ili kuleta ustawi wa
maendeleo tukiwa tumeridhiana na tukiwa tunavumiliana kuweza kufanya
siasa zetu, kwa hiyo tulikotoka ni kuzuri tuliko ni kuzuri zaidi na
tunakokwenda ni kuzuri na muelekeo ni mzuri sana,”amesema Shaka.
Kuhusu
ziara yake kwenye kituo hicho cha redio Shaka amesema Chama Cha
Mapinduzi kimeona kina kila sababu ya kuhakikisha kinaendelea kuimarisha
mahusiano mazuri kati yake na vyombo vya habari nchini, na ili kujenga
mahusiano hayo ameamua kufanya ziara hiyo.
Ametumia nafasi hiyo
kutoa shukrani zake za dhati kwa uongozi wa Zenji FM kwa mchango wake
mkubwa kwa CCM lakini kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Redio yenu imekuwa
ikizungumza na kuhamasisha masuala ya maendeleo katika serikali zote
mbili, na kwa CCM tunatambua mchango wa redio hii na tutaendelea kuuenzi
na kuuheshimu, tumekuja hapa kuwahakikisha kwamba Chama kipo pamoja
nanyi na kwenye changamoto tushirikishane kutafuta ufumbuzi,”amesema
Shaka.
Pamoja na mambo mengine Shaka aliomba wafanyakazi wa redio
hiyo pamoja na msafara wake kusimama kwa dakika moja kwa ajili ya
kumuombea dua aliyekuwa Mkurugenzi na Mwanzilishi wa kituo hicho Mohamed
Seif Hatibu ambaye kwa sasa ni marehemu.
Shaka amesema sababu za
kufanya kumuombea ni kutokana na kuenzi na kukumbuka mchango wake
katika harakati za mapinduzi ya kuanzisha redio binafsi katika visiwa
vya Zanzibar.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...