*Washindi 30 kupewa elimu, watatu zawadi za fedha taslimu
VIJANA 500 wakazi wa Wilaya ya Temeke wenye umri kati ya miaka 18 na 35 wengi wao wakiwa wenye biashara ndogo na wale wenye ndoto kubwa ya kuwa wajasiriamali watakutana katika ukumbi wa manispaa hiyo kwa shindano kubwa linalotarajia kuibua ushiriki wao katika ajira, uchumi binafsi na wa taifa.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Jaji Mkuu wa shindano hilo lenye lengo la kuhamasisha uelewa wa masuala ya fedha na ujasiriamali kwa vijana, Bi. Maida Waziri alisema lengo kubwa la shidano hilo ni kuwatambua vijana wanaochakarika, haijalishi biashara ao ni ndogo kiasi gani, ili waweze kusogezwa mbele zaidi.
Shidano hilo ambalo ni kwa ajili ya vijana wakazi wa Temeke pekee litafanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Temeke Julai 15.
Bi. Maida alisema Akili Ya Pesa Challenge ni mradi wa kijamii wenye lengo la kuwainua zaidi vijana katika kushughulikia masuala ya ujasiriamali.
“Mradi huu una lengo la kubadili tabia ya vijana katika masuala ya ujasiriamali kuwaondoa woga na kuwashawishi washiriki kikamilifu kwa kuzingatia fursa nyingi ambazo zipo,” alisema Maida
Mradi huo unapanga kuwapatia vijana wa Temeke elimu ya ujasirimali, elimu ya fedha na kupewa hamasa ya kukumbatia ujasiriamali na kutengeneza nafasi ya ajira kwao na kwa wengine.
“Kwa kuangalia Temeke pia tunataka kuwajaza na kuwafumbua macho wanaTemeke, hasa vijana dondoo muhimu za biashara, uwekezaji na ujasiriamali uliopo katika eneo hilo,” alisema Bi. Maida.
Bi. Maida katika taarifa yake hiyo alisema viongozi wakuu wa wilaya hiyo akiwemo Mkuu wa wilaya Mheshimiwa Jokate Mwegelo na meya wa manispaa Mh. Abdallah Mtinika wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika kushawishi vijana kutambua nafasi za uwekezaji katika wilaya ya Temeke, hivyo kilichobaki ni kwa vijana wenyewe kuona, kutambua na kushiriki kukuza uchumi wao na wa wilaya.
Temeke imeelezwa kuwa moja ya wilaya Kongwe nchini ambazo zimekuwa na nafasi nzuri kuanzia katika mapambano ya kudai uhuru, utekelezaji wa kilimo, uendelezaji wa michezo na mambo kadha wa kadha ambayo yanaweza kuwezesha ajira na kazi.
Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Menejimenti na maendeleo ya ujasiriamali,Dk Donath R.Olomi, ambaye pia ni jaji wa Akili Ya Pesa Challenge anasema mradi huo imelenga kufungua vichwa vya vijana kuhusu masuala ya fedha na ujasiriamali.
“Tunahitaji vijana wetu wafunguke ili tuweze kusonga mbele na kufikia malengo” alisema.

Watatu watakaochomoza washindi katika shindano hilo la Akili ya Pesa Challenge- Temeke watatia kibindoni jumla ya Sh milioni 6, milioni Tatu ikienda kwa mshindi kwanza , wa pili sh milioni mbili na wa tatu sh milioni moja.
Aidha washidi hao watatu watashindana na washindi wengine nchi nzima kupata mafunzo na thamani kubwa zaidi ya ushiriki na ushindi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...