Na Joseph Lyimo
WILAYA
ya Simanjiro Mkoani Manyara imeongoza kwa asilimia 119 kwa wananchi wa
Mkoa huo kupata chanjo ya UVIKO-19 kwenye wakati huu ambapo zoezi la
wananchi kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya UVIKO-19
likiendelea katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa
mujibu wa matokeo ya uchanjaji UVIKO-19 yaliyotolewa hivi karibuni
kwenye Halmashauri saba za Wilaya za Mkoa wa Manyara, Halmashauri ya
Simanjiro imeongoza kwa kupata asilimia 119.
Halmashauri
ya Wilaya ya Babati, imeshika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 78,
Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ imeshika nafasi ya tatu kwa kupata
asilimia 69 na Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, imeshika nafasi ya nne
kwa kupata asilimia 67.
Halmashauri
ya Mji wa Babati imeshika nafasi ya tano kwa kupata asilimia 58,
Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imeshika nafasi ya sita kwa kupata
asilimia 56 na Halmashauri ya Mji wa Mbulu imeshika nafasi ya saba kwa
wananchi wake kuchanja UVIKO-19 kwa asilimia 54.
Kaimu
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mbaraka Alhaji Batenga amewapongeza
viongozi, wataalamu wa afya na wananchi wa Simanjiro ujumla kwa
kuhamasika na kufanikiwa kuongoza kiwilaya kwenye kushirikia kupata
chanjo ya UVIKO-19.
“DMO
(Mganga mkuu wa Wilaya), wataalamu wa afya na jamii kwa ujumla,
ninawapongeza kwa namna mnavyoshughulikia suala hili la kitaifa kwani
inaonyesha ni namna gani mnajitoa katika kutoa elimu kwa watu katika
kuhakikisha wanashiriki kwa hiyari kupata chanjo,” amesema Batenga.
Mkuu
huyo wa Wilaya ya Kiteto ambaye anakaimu Wilaya ya Simanjiro, amesema
anatarajia wananchi ambao hawajapata chanjo ya UVIKO-19 watashiriki
kupata chanjo hiyo ambayo inaendelea kutolewa na wataalamu wa afya.
“Rais
Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango na Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakituasa wananchi
kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani maradhi hayo bado yapo nchini
hivyo tushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19,” amesema.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga Laizer
amewashukuru wananchi kwa ujumla na wataalamu wa afya kwa namna
walivyotekeleza shughuli hiyo ya zoezi la chanjo ya UVIKO-19.
Amesema
mwitikio wa viongozi na wananchi katika kupokea suala la chanjo ya
UVIKO-19 imesababisha shughuli hiyo iende kama ilivyopaswa na matokeo
chanja yakaonekana kwa Simanjiro kuongoza.
“Niwaombe
viongozi wa dini, wazee wa kimila, viongozi wa kisiasa na serikali na
wananchi kwa ujumla, tushiriki kupata chanjao na yule ambaye bado
hajapata chanjo ya UVIKO-19 apate ili ajilinde na maradhi hayo,” anasema
Mwenyekiti huyo wa Halmashauri hiyo.
Mganga
mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro (DMO) Dkt Aristidy Raphael
amesema halmashauri hiyo imeongoza kwenye uchanjaji mkoani humo kutokana
na mwitikio mkubwa wa jamii uliopo hivi sasa.
“Tunawapongeza
wananchi wa Simanjiro kwa kuitikia hili na kushiriki kupata chanjo ya
UVIKO-19 kwani baada ya kupata elimu na kutambua umuhimu wa chanjo
waliridhia na kukubali kupata chanjo hiyo,” amesema Dkt Raphael.
Ametoa
wito kwa wananchi wa Simanjiro ambao bado hawajashiriki kupata chanjo
ya UVIKO-19, wahakikishe wanapata kwani Serikali kupitia Wizara ya Afya
imetoa matangazo mbalimbali kwa wananchi kupata chanjo ya UVIKO-19.
Amesema
wataalamu wa afya wanatembelea makundi mbalimbali ya wananchi wa
Simanjiro kuanzia wafugaji, wakulima, wachimba madini, wavuvi,
wafanyabiashara na watu wa kada mbalimbali ili wawafikie na kuwahudumia.
Baadhi
ya wananchi wa Wilaya ya Simanjiro, wanaeleza kuwa wamehamasika kupata
chanjo hiyo ya UVIKO-19 ili kujikinga na gonjwa hilo kwani wataalamu wa
afya wamewapa elimu ya kutosha.
Mkazi
wa kitongoji cha Manyara, Elijah Ngao amesema hatua ya wananchi wa
Wilaya Simanjiro kujitokeza kuchanja kwa wingi chanjo ya UVIKO-19
inatokana na hamasa iliyotolewa na wananchi kupatiwa elimu kuwa chanjo
hiyo haina madhara.
“Mara
nyingi kitu kigeni kikitokea kuna baadhi ya watu wanapotosha na
kuzungumza ndivyo sivyo juu ya jambo hilo utadhani wanalitambua kumbe
hawafahamu ila hili la UVIKO-19 wengi wao wamelitambua na kulielewa
ndiyo sababu wamejitokeza kwa wingi kuchanja,” anasema Ngao.
Amesema
baada ya maneno ya uongo na dhana potofu kuonekana kuwa ni propaganda
zisizo na maana yoyote, wananchi wameamua kushiriki chanjo ya UVIKO-19
kwa manufaa yao.
“Mtu
anaona atapata maambukizi ya UVIKO-19 yeye mwenyewe na hayo ni maradhi
ambayo hayana matibabu hivyo ameona hawezi kupata tatizo kisa
kutochanjwa kwa kutosikiliza wataalamu wa afya na kuwasilikiza
wazushaji,” anaeleza.
Mkazi
wa kata ya Shambarai John Issangya anasema wataalamu wa afya wamekuwa
wanafika hadi vijijini na kutoa elimu kwa jamii kIsha kuwapatia chanjo
hiyo ya UVIKO-19.
“Hadi
hivi sasa elimu inaendelea kutolewa kwa jamii huku vijijini na
wanaitikia ushauri wa kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 kwani wanatambua kuwa
ukipata maradhi hayo bila kuchanja utapata matatizo makubwa kwenye
changamoto ya kupumua pindi ukiupata ugonjwa huo,” anasema.
Mkazi
wa kata ya Endiamtu Mashaka Jororo anasema kuwa viongozi na wananchi wa
Wilaya ya Simanjiro kwa pamoja wameungana katika kuhakikisha wanapata
chanjo ya UVIKO-19 ndiyo sababu wakaongoza kushika nafasi ya kwanza.
“Siyo
jambo dogo Simanjiro kushika nafasi ya kwanza kati ya Halmashauri saba
za Wilaya kwa hapa Manyara, binafsi niwapongeze wana Simanjiro kwa
kufanikisha hili na kuongoza,” anasema Jororo.
Anasema
anatarajia wananchi wa wilaya ya Simanjiro wataendelea kupata chanjo ya
kujikinga na janga la UVIKO-19 kwa kuwasikiliza viongozi wa Serikali na
wataalamu wa afya na siyo vinginevyo.
Hivi
karibuni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza hivi karibuni kwenye
tamasha la MZIKI MNENE lililofanyika uwanja wa Nangwanda Mkoani Mtwara
amesema imethibitika kuwa njia ambayo ni salama ya kujikinga na ugonjwa
wa UVIKO-19 ni kupata chanjo kwani ukichanja utakuwa umejikinga na
kuikinga jamii ya watanzania.
Waziri
Ummy amesema Serikali inaendelea kuwalinda wananchi wake katika
maambuzi ya magonjwa mbalimbali kwa kutoa chanjo ikiwemo ya UVIKO-19.
“Sisi
kama Wizara ya Afya tutatumia mbinu mbalimbali ambazo zitakazowafikia
wananchi kama tunavyotumia matamasha haya kutoa elimu na kuhamasisha
wananchi kupata huduma ya chanjo ya UVIKO-19,” anamaliza kwa kusema
Waziri Ummy.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...