*Mkataba wa miaka mitano iliyopita Yanga SC walipata Shilingi Bilioni 5.2

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KAMPUNI ya Michezo ya Kubashiri ya Sportpesa imeingia mkataba wa makubaliano wenye thamani ya Shilingi Bilioni 12.33 na Yanga SC kwa kipindi cha miaka mitatu, baada ya mkataba wa awali wa miaka mitano kutamatika mwaka huu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi  ya Sportpesa, Abbas Tarimba amesema mkataba huo utakuwa wa miaka mitatu wenye thamani ya kiasi hicho cha fedha huku Klabu hiyo ikitarajiwa kupata Shilingi Bilioni 4 kila mwaka.

“Tumeingia mkataba huu na Yanga SC ambao imepanda thamani kubwa, tofauti na mkataba uliopita, walikuwa wanapata Bilioni 1 kwa mwaka, sasa hivi tumeongeza thamani kwa kuwapa Shilingi Bilioni 4 kwa kila mwaka kwenye sehemu ya mkataba wetu”, amesema Tarimba.

“Yanga SC ikishinda ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao watapata bonasi ya Shilingi Milioni 150 tofauti na zamani walikuwa wanapata Shilingi Milioni 100, lakini kwenye Michuano ya ASFC wakifika Fainali watapata bonasi la Shilingi Milioni 75 na wakishinda Ubingwa wa Michuano hiyo watapata Shilingi Milioni 112”, ameeleza Tarimba 

Kwa upande wake, Rais wa Klabu hiyo, Mhandisi Hersi Said ameshukuru Uongozi wa Kampuni hiyo ya Sportpesa kwa kuingia makubaliano ya mkataba huo na Klabu ya Yanga ambayo inatarajiwa kufanya vizuri msimu ujao kutokana na hamasa hiyo sanjari na usajili ulifanywa kuelekea msimu ujao wa mashindano.

“Haikuwa rahisi kufika makubaliano haya ambayo leo, sisi na Sportpesa tunasaini makubaliano haya, tunaamini kazi kubwa imefanywa na Uongozi wa Yanga SC chini ya Dkt. Mshindo Msolla ambaye ni Mwenyekiti Mstaafu na Wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji”, amesema Mhandisi Hersi.

“Mafanikio haya ya Uongozi uliopita kwa kiasi kikubwa yamesababisha Yanga SC kutwaa mataji matatu ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Soka Tanzania Bara na Michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) msimu wa 2021-2022, tunaamini msimu ujao tutafanya makubwa zaidi kwa Uongozi wa sasa uliopo madarakani”, ameeleza Mhandisi Hersi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Sportpesa, Abbas Tarimba (Kulia) na Rais wa Klabu ya Yanga, Mhandisi Hersi Said (Kushoto) wakionyesha mkataba mpya uliosainiwa leo baina ya Kampuni hiyo na Klabu hiyo, mkataba huo una thamani ya jumla ya kiasi cha Shilingi Bilioni 12.33 kwa kipindi cha miaka mitatu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...