Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
14/07/2022 Wanachama wa Chama cha kuweka Akiba na Mikopo (SACCOS) cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wameshauriwa kuendelea kuhifadhi fedha katika SACCOS hiyo ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima yanayoweza kujitokeza pale mtu anapokuwa na fedha mfukoni.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Ushirika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Donard Kibuti wakati wa kikao cha kwanza cha kujadili bajeti ya SACCOS hiyo kilichofanyika jana katika ukumbi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam
“Jitahidini kutumia hii SACCOS kama sehemu ya kuleta faida ya kiuchumi katika maisha ya kila mmoja kwa kuweka akiba kwani ni sehemu ambayo mtu huwezi kutoa pesa kirahisi tofauti na kuhifadhi fedha benki ambapo wakati wowote ukizihitaji ni rahisi kuzichukua”,.
“SACCOS zinasaidia kupata mkopo wenye riba naafuu na wa dharura hivyo ni muhimu kuwekeza wakati bado tuna nguvu kwani hata leo ukiwa haupo fedha uliyoiwekeza katika SACCOS itasaidia familia zenu”, alisema Kibuti.
Kwa upande wake Afisa Ushirika kutoka ofisi ya Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Olivia Kaiza amewataka viongozi wa SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kuandaa taarifa ya SACCOS hiyo kila baada ya miezi mitatu kwani kwa kutokufanya hivyo watatakiwa kulipa faini ya shilingi laki tano.
“Nawapongeza kwa kufanya kikao hiki cha kwanza tangu kuanzishwa kwa SACCOS hii mwaka 2020, lakini niwaombe kuhakikisha kuwa taratibu zote za kuendesha SACCOS zinafuatwa ili muwe katika mstari unaotakiwa”, alisema Olivia.
Aidha Olivia aliwataka viongozi wa SACCOS hiyo kufuatili leseni ya SACCOS yao ili waweze kutambulika na Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Tulizo Shem aliwaahidi wajumbe wa SACCOS hiyo kuwa baada ya kikao hicho viongozi watafuatilia taratibu zote zilizobaki za kuendesha SACCOS hiyo.
“Niwahakikishie wanachama wa SACCOS yetu kuwa viongozi wenu tupo tayari kuwatumikia na naomba niwaahidi kuwa leo tunaanza kufuatilia matakwa ya kisheria yanayohitajika katika kuendesha SACCOS yetu”,.
“Sambamba na kukamilisha matakwa ya kisheria ya SACCOS tunaendelea na jitihada za kuhamasisha wananchama wapya ili SACCOS yetu iendelee kukua na kuwa yenye tija katika maisha yetu ya kila siku”, alisema Dkt. Shem.
Mwenyekiti wa SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Tulizo Shem akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa SACCOS hiyo baada ya kikao cha kwanza cha kujadili bajeti kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Picha na: JKCI
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...