…………………………….
Na mwandishi wetu, NCAA
Waziri wa maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) leo tarehe 13 Julai, 2022 amefungua barabara mpya iliyojengwa kwa teknolojia ya mawe kutoka Seneto hadi bonde la Ngorongoro Kreta yenye urefu wa Kilomita 4.2.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Barabara hiyo Waziri Chana ameupongeza Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kukamilisha barabara hiyo ambayo ndio njia kuu ya watalii kuelekea kwenye kivutio maarufu cha Kreta ya Ngorongoro.
“Nawapongeza NCAA kwa kukamilisha mradi huu kwa wakati, baada ya uzinduzi wa filamu ya Royal tour iliyofanywa na Mhe Rais Mama Samia Suluhu Hassan idadi ya wageni wanaotembelea hifadhi zetu imeongezeka sana, tunafarijika kuwa wanavyokuja wanakuta Serikali imeshafanya jitihada kubwa hasa katika uboreshaji wa Moundombinu” amesisitiza Balozi Dkt. Chana.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Needpeace Wambuya ameeleza kuwa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 4.2 imegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.7 na imejengwa kwa teknolojia ya mawe ambayo ni rafiki kwa mazingira hasa katika maeneo ya Hifadhi.
Ameongeza kuwa pamoja na ujenzi wa barabara hiyo, NCAA inaendelea kuboresha barabara nyingine ndani ya hifadhi ili ziendelee kupitika msimu wote wa mwaka.
Msimamizi wa Mradi huo Kamishna msaidizi Mwandamizi wa Uhidadhi Mhandisi Daniel Chegere amebainisha kuwa ujenzi wa barabara za mawe ni wa uhakika unaoweza kudumu kwa muda wa miaka 100 tofauti na barabara za lami ambazo hudumu kwa kati ya miaka 10 hadi 20 pekee.
Ameendelea kuongeza kuwa teknolojia ya barabara ya mawe ni nafuu kulinganisha na lami ambapo kilomita moja ya barabara ya mawe inagharimu wastani wa shilingi Milioni 400 hadi milioni 450 kulinganisha na kilomita moja ya lami ambayo gharama yake ni kati ya bilioni moja hadi bilioni 1.5.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TATO Wilbard Chambulo ameeleza kuwa, kukamilika kwa barabara hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa usafirishaji wa wageni na kumaliza changamoto iliyokuwepo awali ya ubovu wa barabara na baadae wageni kulazimika kutumia barabara moja kwenda na kurudi katika bonde la Kreta ya Ngorongoro.
“Hii imekuwa neema, tunaishukuru Serikali kwa kujenga barabara hii na kuikamilisha, sisi kama wadau wakubwa tumefarijika sana kwa kuwa hatutabanana tena kwenye njia moja kama awali wakati njia hii ilivyokuwa inajengwa” amefafanua Chambulo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...