Rahma Khami Maelezo
Masheha na Madaktari wa Wilaya ya Magharibi A’na B’wametakiwa kuhamasisha wananchi wao kushiriki katika zoezi la chanjo ya uviko 19 ili kujikinga na maradhi hayo.
Akizungumza katika uzinduzi wa kuhamasisha chanjo ya Corona katika Uwanja wa Hospitali ya Kianga, Naibu Waziri wa Afya Hassan Hafidh amesema takwimu zinaonesha wilaya hizo bado hazijahamasika katika kuchanja chanjo hiyo jambo ambalo linarejesha nyuma juhudi za serikali katika mapambano hayo .
Amesema kuwa Serikali za mitaa kwa kushirikiana na wafanyakazi wa huduma za afya katika shehia zao (Afya ya jamii) kupita kila sehemu na kila nyumba kuhamasisha jamii ili waweze kuchanja.
Aidha amefahamisha kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ina jukumu la kuhakikisha wanalinda na kuwakinga wananchi wao kutokana na maradhi mbalimbali kwa kutafuta dawa za kupambana na maradhi ikiwemo chanjo ya uviko 19 ili Zanzibar ibaki salama.
“Lazima tuhakikishe tunawalinda na kuwakinga wananchi wetu katika kupambana na maradhi ya uviko 19 kwani maradhi hatari na yanasambaa kwa kasi zaidi hivyo tujitokeze tukachanje ili tujikinge” alisema Naibu Waziri.
Hata hivyo Naibu amewataka wananchi wa wilaya hizo kujitokeza kwa wingi kupata chanjo hiyo, kwani wanaopata maambukizi ni wale ambao hawajapata chanjo na kinga ni bora kuliko tiba.
Nae Mratibu wa chanjo ya Abdulhamid Ameir Saleh amesema kuwa Wilaya ya Magarib A’ na B’ni miongoni mwa wilaya sita ambazo hazikufanya vizuri katika kushiriki chanjo hiyo jambo amba linahatarisha maisha ya wananchi.
Amefafanua kuwa kwa Wilaya hizo kuna mikakati maalum ya kuhamasisha wananchi kujikinga kwani bado zipo chini ya asilimia 24 hivyo endapo watajitokeza kuchanja itasaidia kasi ya maambukizi.
Nae Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt Andamichel Ghirmay ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuamua kufanya uzindizi katika wilaya hizo na kuendeleza mashirikiano yaliopo katika sekta ya afya.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Hafidh akizungumza na masheha na madaktari wa Wilaya ya Magharibi A’na B’ juu ya umuhimu wa chanjo ya Uviko 19 wakati wa uzinduzi wa kuhamasisha chanjo hiyo huko Hospitali ya Kianga Wilaya ya Magharibi "A" Mkoa wa Mjini Magharibi.
Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt Andamichel Ghirmay akitoa neno la shukurani kwa Wizara ya Afya Zanzibar wakati wa uzinduzi wa kuhamasisha chanjo ya Uviko 19 huko Hospitali ya Kianga Wilaya ya Magharibi "A" Mkoa wa Mjini Magharibi.
Mratibu wa chanjo ya Uviko 19 Abdulhamid Ameir Saleh akizungumza na masheha na madaktari wa Wilaya ya Magharibi A’na B’ juu ya umuhimu wa chanjo ya Uviko 19 wakati wa uzinduzi wa kuhamasisha chanjo hiyo huko Hospitali ya Kianga Wilaya ya Magharibi "A" Mkoa wa Mjini Magharibi.
Wanafunzi wa skuli za sekondari Wilaya ya Magharibi "A" wakifuatilia hafla ya Uzinduzi wa kuhamasisha chanjo ya UVIKO 19 huko Hospitali ya Kianga Wilaya ya Magharibi "A" Mkoa wa Mjini Magharibi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...