MKURUGENZI wa Mipango, Fedha, Utawala na sheria wa shule za Atlas, Didace Kanyambo amekanusha taarifa za Uongo kuhusu shule za Atlas za jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Agosti 21, 2022. Amesema kuwa taarifa hizo ni za uongo zenye kujaa chuki, upotoshaji, zenye lengo la kuichafua shule, kuleta taharuki na kuishushia shule hadhi na heshima mbele ya macho ya jamii.

Amesema "Mnamo Agosti 19, 2022 mtu anaejitambulisha kama Mchungaji wa Taifa Nabii MIKAYA KOMANDO MASHIMO alitoa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa shule yetu ya Atlas Madale imekamata wanafunzi wa miaka 12 na kuwafungia kwenye mahabusu iliyofungiliwa na shule kwaajili ya wanafunzi ambao hawajakamilisha ada.

Pia alisema kuwa mtoto hatoruhusiwa kwenda nyumbani na huwa mtoto hali wala hanywi."

Kanyambo amesema taarifa hizo zipuuzwe na hazina ukweli wowote.
"Shule hii ni zao la sheria ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na kwa msingi huo inaendeshwa kwa kufuata sheria, taratibu, kanuni na miongozo inayotolewa na mamlaka za serikali." Amesema Kanyambo

Amesema shule hiyo haijawahi kuwa na mahabusu na hawawezi kuwa na mahabusu kwasababu ni kinyume na sheria na taratibu za nchi.

"Naomba ieleweke kwamba sisi kama wadau wa elimu kazi yetu ni kutoa elimu na malezi na si vinginevyo.

Mtu anaejitambulisha kama Mchungaji wa taifa Nabii Mikaya hatumfahamu na wala hana mtoto katika shule za Atlas na hajawahi kusomesha mtoto katika shule zetu, kwa hiyo alitoa taarifa za kupikwa zenye nia ovu, hila na chuki binafsi dhidi ya shule ya Atlas Madale kwa lengo la kuichonganisha na jamii pamoja na serikali." Amesema Kanyambo

Amesema Kuwa Agosti 18, 2022 wanafunzi wa madarasa ya mitihani ya taifa (darasa la nne na la saba) walifunga shule ili wanafunzi na wafanyakazi warejee makwao kujiandaa na zoezi la kitaifa la sensa litakalofanyika Agosti 23, 2022 kama ilivyoelekezwa na Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi kuwa kabla ya tarehe ya sensa shule zote ziwe zimefungwa ili kufanikisha zoezi hilo muhimu.

"Siku ya Alhamis tarehe 18/08/2022 tuliwaalika wazazi/walezi kuja kuchukuwa watoto wao kama ulivyo utaratibu wetu siku zote kwamba mtoto hawezi kuondoka shuleni bila kufuatwa na mzazi/mlezi anaefahamika na ofisi ya Mkuu shule ili kujiepusha na changamoto zinazoweza kujitokeza kwa kumkabidhi mtoto kwenye mikono isiyo salama.

Wazazi/walezi waliitikia wito na walifuata utaratibu wa shule wa kuhakikiwa na ofisi ya Mkuu wa shule kabla ya kumchukuwa mtoto ikiwa pamoja na kupewa taarifa zake za maendeleo ya taaluma, kuhakiki kama mzazi amekamilisha malipo ya ada na michango iliyopitishwa kwenye vikao vya kamati ya shule na wazazi. Kwa mzazi ambae hakuweza kutimiza wajibu wake kwa wakati alipewa nafasi ya kujieleza na kuahidi namna ya kukamilisha malipo hayo na kisha kupewa mtoto wake. Zoezi liliendelea hadi saa moja jioni na watoto wote walirejea makwao." Ameeleza Kanyambo

Amesema taasisi imesikitishwa na kuumizwa na taarifa hizo potofu zilizotolewa na anaejitambulisha kama Mchungaji wa taifa Nabii Mikaya Komando Mashimo.

"Kwa hali hiyo kama taasisi tutashirikiana na vyombo vya dola ili kuchukuwa hatua stahiki za kisheria dhidi yake na washirika wake wenye nia ovu na roho mbaya ya kuchafua taasisi yetu."

Aidha amewaomba wananchi wote wapuuze taarifa hizo ambazo hazina ukweli wowote.

Amesema taasisi ya shule ya Atlas Madale na shule zote za Atlas wako imara na wanaendesha shule kwa kufuata sheria, taratibu, kanuni na miongozo inayotolewa na Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi. Pia wanaendelea kutoa huduma katika ubora wa hali ya juu.

Kanyambo amemalizia kwa kusema wanaendelea kuwaheshimu na kuwathamini mteja wao na serikali kwa ujumla.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...