Dar es Salaam: Octoba 28, 2022: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw Amos Makalla amezindua tawi jipya la Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) lililopo eneo la Kibada wilayani Kigamboni huku akitoa wito kwa wakazi wa wilaya hiyo na maeneo jirani kuchangamkia fursa za kiuwezeshaji kiuchumi zinazoletwa na ujio wa hiyo wilayani humo.
Hafla ya uzinduzi wa tawi hilo ilifanyika kwenye tawi hilo mapema hii leo na kuhudhuliwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa chama na serikali, viongozi waandamizi wa benki hiyo na wafanyakazi, wawakilishi wa jumuiya ya wafanyabiashara pamoja na wananchi
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Bw Makalla alisema mitaji ya fedha ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi hivyo uwepo benki hiyo wilayani humo utakuwa na tija zaidi iwapo tu wakazi wa wilaya hiyo wataitumia vema fursa hiyo.
“Najua fika kwamba kusogezewa karibu huduma za kifedha ikiwemo benki kama hivi ni jambo moja na kutumia ipasavyo uwepo wa huduma hizi ni jambo lingine. Ndio maana nawaomba sana wana Kigamboni kutumia vema uwepo wa benki kama hii ya NBC kwa kutunza akiba zenu na pia kukopa ili kuwekeza na kukuza biashara zenu,’’ alisema.
Hata hivyo Bw Makalla alitoa rai kwa benki hiyo kuendelea kubuni mipango mbalimbali ya utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutumia benki sambamba na kubuni huduma zinazowagusa wananchi wa wenye hali ya kawaida kiuchumi ili waweze kutumia vema fursa na huduma zinazotolewa na benki hiyo.
“Nafahamu Benki ya NBC mmekua mkibuni njia mbadala za kuwahudumia wateja kupitia njia mbalimbali ikiwemo kupitia mawakala na huduma kupitia simu yaani NBC Kiganjani, NBC Shambani na nyingine nyingi, Nawapongeza sana. Ila naomba sana endeleeni kuwaelimisha wateja wenu namna ya kutumia fursa za kibenki na kujiweza na kujikomboa kiuchumi.’’ Aliomba.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bi Fatuma Nyangasa aliishukuru benki ya NBC kwa kusogeza huduma zake wilayani Kigamboni kwa kuwa itarahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki ambazo kwa kiasi kikubwa wilaya hiyo inategemea kuzipata kupitia wilaya ya Temeke.
“Wilaya ya Kigamboni kwa sasa inakuwa kwa kasi sana na wakazi wanaongezeka kila siku huku shughuli za kiuchumi pia zikiongezeka. Ongezeko hili la watu na ukuaji wa kiuchumi unahitaji kwenda sambamba na huduma mbalimbali ikiwemo hii ya kifedha…tunawashukuru sana na NBC kwa kuliona hili,’’ alisema.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi alisema benki hiyo ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 30 inaendelea kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuwawezesha wajasiliamari na wakulima na wazalishaji wengine katika sekta za uchumi kwa kwa kutoa mitaji ya kifedha na mikopo nafuu.
“Jitihada hizi tunazitekeleza kwa urahisi zaidi kutokana wingi wamatawi yetu katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Tawi hili jipya la Kigamboni tunalolifungua leo linafanya Benki ya NBC sasa kuwa na jumla ya matawi 16 mkoani Dar es Salaam pekee huku tukiwa na matawi 47 kote nchini.’’
“Kupitia matawi haya tumekuwa tukihudumia makundi yote ya jamii ikiwemo taasisi za serikali, watumishi wa serikali, wafanyabiashara, wanafunzi sambamba na kukusanya maduhuli ya serikali kupitia Mfumo wa Ukusanyaji wa Fedha za Umma (GePG) na kodi kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).’’ Alitaja.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw Amos Makalla (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (kushoto) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bi Fatma Nyangasa (wa pili kulia) wakimsikiliza Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa Benki ya NBC, Elibariki Masuke wakati akieleze kuhusu kuhusu tawi jipya la benki ya NBC wilayani Kigamboni wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa tawi hilo iliyofanyika wilayani humo leo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...