Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
27/10/2022 Wataalamu wa Afya 65 kutoka hospitali mbalimbali hapa nchini wanashiriki mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum na mahututi yanayotolelewa na madaktari bingwa wa Moyo kutoka Shirika la Cardiostart International la nchini Marekani.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo yamehusisha mafunzo ya kutumia vifaa mbalimbali vya matibabu vinavyotumika katika kutoa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji huduma maalum na mahututi.
Akizungumza na vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Peter Kisenge alisema JKCI imeona umuhimu wa wataalam wa afya kupata mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi kwasababu wagonjwa hao wako katika hali ya kuumwa sana na ni rahisi kwao kupoteza maisha ghafla kama hawatapata huduma vizuri.
“Wagonjwa wetu wengi wanakuja wakiwa katika hali mbaya hivyo mafunzo haya kwetu sisi ni ya muhimu kwani wagonjwa mahututi wasipohudumiwa vizuri na kwa haraka wanaweza wakapoteza maisha yao,”.
“Tumewaalika wataalamu mabingwa wa moyo kutoka nchini Marekani ambao kwa siku tatu watawapa wataalamu wetu uwezo na ujuzi wa hali ya juu na baada ya mafunzo haya watalamu wetu watapeleka utaalam huo kwa wenzao ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo haya,” alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt. Kisenge alisema Serikali ya awamu ya sita imewekeza kwa kiasi kikubwa katika vifaa tiba kwenye vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU) hivyo kupitia mafunzo hayo wataalamu wa afya watapata pia nafasi ya kufundishwa namna ya kutumia mashine hizo na kuzitunza kwa maslahi ya nchi.
“Mafunzo haya yanaenda kuwa endelevu hapa kwetu kwani kila baada ya miezi mitatu wataalam wetu watapata mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na namna ya kutumia mashine za kuwahudumia wagonjwa hao ili kwa pamoja tutoe huduma bora na kulinda vifaa vyetu vya matibabu,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Angela Muhozya alisema JKCI imeamua kuanzisha mafunzo hayo baada ya kuona uhitaji mkubwa uliopo nchini katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi.
“Tumedhamiria baada ya mafunzo haya wataalam wetu wataenda kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi katika kiwango cha ufanisi mkubwa zaidi na kupunguza vifo vinavyotokea kwa wagonjwa hao”, alisema Dkt. Angela.
Dkt. Angela ambaye pia ni mratibu wa mafunzo hayo alisema JKCI ni mdau mkubwa katika eneo la kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi kwani wagonjwa wengi wa moyo wanaofika katika Taasisi hiyo wanakuwa katika hali mbaya lakini pia wagonjwa wa moyo wanaofanyiwa upasuaji wa moyo huwa katika hali ya umahututi hivyo uhitaji kupatiwa huduma hizo.
“Tupo na wataalam wabobezi wa magonjwa ya dharura na mahututi ambao wanatupa mafunzo kwa kiwango cha hali ya juu, tunaamini ndani ya siku hizi tatu wataalamu wetu walioshiriki mafunzo haya watakuwa na elimu ya ziada watakayoenda kuitumia katika maeneo yao ya kazi,” alisema Dkt. Angela.
Akizungumzia mafunzo hayo Daktari bingwa wa wagonjwa wanaohitaji huduma ya dharura na mahututi kutoka Shirika la Cardiostart International la nchini Marekani Richard Harper alisema madaktari kutoka shirika hilo wamekwenda JKCI kwa ajili ya kuwasaidia wataalam wa afya hapa nchini ili waweze kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba.
“Nimefurahi kuona wataalam wa afya walioshiriki mafunzo haya wanajitoa na kutamani kujua zaidi namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi, tunaenda kuwapa mafunzo ya hali ya juu ambayo yataleta mabadiliko katika kutekeleza majukumu yao,”alisema Dkt. Richard.
Naye Daktari kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) Issa Kisoma alisema amevutiwa kushiriki mafunzo hayo kwasababu katika eneo lake la kazi amekuwa akikutana na wagonjwa wanaohitaji kupatiwa huduma ya dharura hivyo kuona umuhimu wa kuongeza ujuzi katika eneo hilo.
“Wagonjwa ninaokutana nao katika eneo langu la kazi wanahitaji kupatiwa huduma ya dharura kwa usahihi ili kuokolewa maisha yao, hivyo natamani sana nisikosee kuwapatia huduma na kupoteza maisha yao ndio maana nikaona nami nishiriki mafunzo haya ili niokoe maisha ya wagongwa ninaowahudumia,”.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...