JESHI la Zimamoto na Uokoaji limetekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan la kumpokea Majaliwa Jackson Samweli ambaye aliyetoa msaada kwa waliopata ajali ya Ndege ya Precision Air iliyotokea katika ziwa Victoria.
Katika Taarifa ya Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kamishna Jenerali John Masunga iliyotolewa leo Novemba 7,2022 na Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Makao Makuu Dodoma, SACF - Puyo Nzalayaimisi imesema kuwa Majaliwa anatarajiwa kuanza mafunzo ya Zimamoto na Uokoaji pamoja na ya Uaskari katika Chuo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kilichopo Chogo Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga.
Ikumbukwe kuwa tarehe Novemba 06, 2022 ilitokea ajali ya kuanguka kwa Ndege ya Precision Air katika Ziwa Victoria, ajali hii ilisababisha majeruhi na vifo. Majaliwa alionesha ujasiri wa hali ya juu, kwa kuokoa wahanga 24 wa tukio hilo.
"Kamishna Jenerali anatoa shukrani za dhati kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Taasisi za Umma na Binafsi, pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Kagera kwa ushirikiano mkubwa waliotoa katika zoezi la uokoaji katika ajali hiyo."
Pia Kamishna Jenerali anatoa pole kwa Wafiwa wote na kuwaombea faraja katika kipindi hiki kigumu wanachopitia, anawatakia majeruhi wote afya njema.
Anawasihi Wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kuokoa Maisha ya watu na mali dhidi ya majanga mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...