Mkurugenzi Mkuu Rasilimali Watu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Ruth Simba akikabidhi cheti cha kutambua mchango wa mkufunzi Dkt. Aloys Rugazia katika hafla ya kuhitimisha mafunzo kwa wadau wa Mafuta na gesi yaliyofanyika jijini Arusha hivi Karibuni.Moja Kati ya wakufunzi wa mafunzo ya mafuta na gesi, Dkt. Aloys Rugazia akitoa mafunzo kwa wataalamu wa sekta hiyo hivi karibuni jijini Arusha
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi za Udhibiti wa huduma za Mafuta na Umeme kwa nchi sita za Afrika Mashariki (EREA) Dkt. Geoffrey Mabea akizungumza na wadau wa mafuta na gesi wakati wa mafunzo kwa wataalamu wa mafuta na gesi 230 kutoka nchi 27 Afrika kutambua namna ya kuandaa mikataba inayohusu sekta hiyo ili kujiinua na kuchangia pato la Taifa.
Kushoto ni Dkt. Shirley Baldwin Mushi akipokea cheti kutoka kwa Mkurugenzi wa Mafunzo na Rasilimali watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Ruth Mtoi Simba cha kutambua mafunzo aliyatoa kwa wadau wa Mafuta na gesi yaliyofanyika jijini Arusha.
Baadhi ya Wadau wa Mafuta na Gesi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada kumalizika kwa mafunzo ya Mafuta na Gesi yaliyofanyika jijini Arusha.
Na Karama Kenyunko, Michuzi Blog
TAASISI za Udhibiti wa huduma za Mafuta na Umeme kwa nchi sita za Afrika Mashariki (EREA) iliyo chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), imesema mpaka sasa imetoa mafunzo kwa wataalamu wa mafuta na gesi 230 kutoka nchi 27 Afrika.
Imesema mafunzo hayo yanalenga kuwafanya wataalamu watambue namna ya kuandaa mikataba inayohusu mafuta na gesi na namna watakavyoshiriki kuinua sekta ya mafuta na gesi na kuchangia pato la taifa.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa EREA, Dkt Geoffrey Mabea wakati akizungumzia mafunzo wanayoyatoa kwa wadau wa mafuta na gesi, mafunzo hayo yamefanyika jijini Arusha.
"Mafunzo haya yamekuwa yakitolewa katika nchi mbalimbali lakini sisi tuliona tuyafanyie hapa kwetu kwa kuwatumia watalaam wa ndani Dkt. Aloys Rugazia na Dkt. Shirley Mushi ambapo tumeweza kuwakutanisha wataalamu wa nchi za Tanzania na Kenya," amesema Dkt. Mabea.
Ameongeza kuwa huu ni mwaka wa pili wanatoa mafunzo ya uelewa kuhusu sekta hiyo na mpaka sasa wataalamu 230 wamenufaika na mafunzo wanayoyatoa kupitia mtandao na chuoni.
Hata hivyo, amesema katika mafunzo yaliyofanyika Novemba 14-18, 2022 wataalamu hao walijadiliana kwa kina kuhusu uchakataji wa mafuta ghafi na gesi chini ya wakufunzi toka hapa hapa Tanzania, Dkt. Aloys Rugazia na Dkt. Shirley Mushi na kushauri haja ya kuwepo kwa mitambo ya Kuchakata Mafuta (Refinery) katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili nchi zipate manufaa yakuchakata Mafuta nyumbani badala yakuagiza Mafuta ambayo yamechakatwa tayari.
Dkt. Mabea ameeleza kuwa biashara ya mafuta imekuwa changamoto kubwa kutokana na gharama zake hivyo wangekuwa na mitambo ya kuchakata mafuta ghafi ingesaidia nchi za Afrika Mashariki kufanya biashara wenyewe na hivyo kupunguza utegemezi na kudhibiti bei za Mafuta na mbolea zitokanazo na Mafuta ghafi.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo ina jukumu la kuwaleta pamoja wadhibiti kwa lengo la kupandisha miundo mbinu ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kusaidia nchi hizo kuwa na misingi bora ya udhibiti na kutekeleza wajibu wao kwa kuwa na wataalamu wengi.
Amesema wameanzisha Chuo kinachotoa mafunzo kwa wadhibiti kilichopo Arusha, ambacho kinatoa mafunzo kuhusu nishati za mafuta na gesi na lengo ni kuwaelimisha namna ya kuchimba na kuchakata gesi kwa matumizi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...