Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHIRIKA lisilo la kiserikali la AKO Ujerumani kupitia Tawi lao la AKO Tanzania Community Support limekabidhi mradi wa vyoo vya kisasa kwa wanafunzi wa shule ya msingi Kambi ya Chokaa Kata ya Naisinyai, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Mkurugenzi wa AKO Tanzania Community Support Hilda Kimath akizungumza wakati wa kuvikabidhi amesema vyoo hivyo vimetumia kiasi cha shilingi milioni 68.
Kimath amesema vyoo hivyo vina matundu 14 vitakavyotumiwa na wasichana matundu nane na wavulana matundu sita.
"Kwenye matundu nane vya wasichana kipo kimoja cha walemavu na matundu sita ya wavulana kipo kimoja cha walemavu pia," amesema Kimath.
Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Laizer amelishukuru shirika la AKO Tanzania kwa kuwajengea wanafunzi hao vyoo hivyo kwani wameisaidia serikali kutimiza wajibu wake.
Afisa elimu vifa na takwimu wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Abdalah Hamis amewataka walimu na wanafunzi kuhakikisha wanatunza miundombinu ya vyoo hivyo ili vidumu muda mrefu.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Praxeda Tarimo amesema AKO Tanzania kabla ya kujenga vyoo hivyo pia wametoa misaada mbalimbali ikiwemo ujenzi wa darasa la awali.
“Pia AKO Tanzania wamesaidia ujenzi wa majiko ya wanafunzi wa darasa la awali na shule ya msingi pia wamefanikisha maji shuleni, chakula kwa wanafunzi, printa na mashine ya photocopy,” amesema Tarimo.
Mwanafunzi wa darasa la sita wa shule ya msingi Kambi ya Chokaa, Christina Julius amesema wanawashukuru AKO Tanzania kwa kuwajengea vyoo hivyo kwani vya awali vimechakaa.
“Sasa hivi tunajisitiri vyema tukiwa faragha na pia tumetengewa eneo maalum la kubadili taulo za kike kwa wale wasichana wakubwa waliopevuka,” amesema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...