Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Wafaransa wamekosa Kombe la Dunia 2022 wakiwa wamecheza Fainali ya Michuano hiyo mara mbili mfululizo yaani mwaka 2018 na 2022. Ufaransa chini ya Kocha Mkuu, Didier Deschamps, mwaka 2018 walitwaa ubingwa wa Michuano hiyo mbele ya Croatia kwa kuwafunga mabao 4-2 nchini Russia.

Mashindano ya mwaka huu wa 2022, yaliyofanyika nchini Qatar, Argentina wametwaa ubingwa wa Mashindano hayo baada ya ushindi wa jumla ya mikwaju ya Penalti 4-2 dhidi ya Kikosi hicho cha Kocha Deschamps katika mchezo wa Fainali uliopigwa katika dimba la Lusail International.

Mchezo huo wa Fainali, Argentina na Ufaransa walilazimika kwenda kwenye hatua ya mikwaju ya Penalti baada ya sare ya mabao 3-3 katika dakika 120’ za mtanange huo. Dakika hizo 120’ timu zote zilionyesha kiwango bora na dunia kushuhudia Fainali ya kiwango cha hali ya juu katika ardhi ya Falme za Kiarabu,

Mashabiki wengi wa Soka ulimwenguni waliokuwa uwanjani zaidi ya Elfu 80, na wale wasiokuwa uwanjani waliwashuhudia na kuwatazama kwa karibu Nyota wanaocheza Klabu ya Paris Saint-Germain FC ya Ufaransa, Mshambuliaji Kylian Mbappe na Lionel Messi ambao wameonyesha kiwango bora katika mchezo huo.

Licha ya kuwepo Nyota wengine walioleta hamasa na hamsha hamsha katika Fainali hiyo, kina Angel Di Maria, Rodrigo De Paul na Alexis Mac Allister kwa upande wa Argentina pia na Randal Kolo Muani, Marcus Thuram na Kingsley Coman kwa upande wa Ufaransa, tulishuhudia mchezo wa aina yake katika dimba hilo la Lusail.

Kocha Deschamps alilazimika kufanya mabadiliko ya mapema sana kuwatoa Olivier Giroud na Ousmane Dembélé baada ya timu hiyo kuwa nyuma kwa mabao 2-0 katika kipindi cha kwanza. Wakiwa nyuma kwa mabao 2-0 kipindi cha pili walirudi na nguvu mpya na hali mpya ambapo walifanikiwa kusawazisha mabao hayo.

Mshambuliaji Kylian Mbappe alifunga mabao matatu peke yake katika mtanange huo, alifunga mabao mawili ya mkwaju wa Penalti na bao moja alifunga kwa ‘shuti kali’ lililomshinda Golikipa wa Argentina, Emiliano Martìnez na kujaa wavuni.

Baada ya kufunga mabao hayo nane katika Michuano hiyo, Mbappe anakuwa Mshambuliaji aliyefunga mabao mengi zaidi akiungana na Gerd Müller wa Ujerumani aliyefunga mabao 10 katika Fainali za Kombe la Dunia 1970 nchini Mexico, huku Ronaldo de Lima aliyefunga mabao nane katika mashindano ya mwaka 2002, Korea na Japan.

Katika usiku huo, Mbappe alifunga jumla ya mabao manne peke yake, licha ya kufunga mabao matatu katika dakika 120’ alifunga pia Penalti moja katika hatua ya mikwaju ya Penalti. Hivyo, Mbappe alifikisha jumla ya mabao nane katika mashindano hayo, na kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora wa mashindano (FIFA Golden Boot).

Katika tuzo nne zilizotolewa katika Fainali za mashindano hayo ya dunia, Ufaransa walipata tuzo moja pekee ya Mfungaji Bora wa mashindano, huku Mchezaji Bora akiwa Lionel Messi, Golikipa Bora, Emiliano Martinez na Mchezaji Bora Chipukizi ni Enzo Fernandez.

Nahodha wa Argentina, Lionel Messi aliweka nia ya kutwaa ubingwa wa Dunia na huenda akastaafu kucheza timu ya taifa na kukosekana kwenye Michuano ijayo ya mwaka 2026, Messi amewahi kutwaa ubingwa wa vikombe mbalimbali maarufu kwenye ngazi ya Klabu sanjari na ngazi ya timu za taifa, katika historia yake ya soka lilibaki taji la Kombe Dunia pekee.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...