Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Mhe. Aswege Kaminyonge akizungumza leo (12.12.2022) Mjini Maswa, wakati akifungua rasmi mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa ugani (hawapo pichani) kutoka mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera na kuwataka maafisa hao kuwasaidia wafugaji kwa kuwapatia elimu ya ufugaji na kuipatia mifugo yao chanjo ili kufuga kwa tija. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Picha ya pamoja ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Mhe. Aswege Kaminyonge baada ya kufungua mafunzo rejea ya siku mbili kwa maafisa ugani kutoka Kanda ya Ziwa Mashariki inayohusisha mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, mafunzo haya yameandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo yanafanyika katika awamu ya pili kwenye kanda tano nchini. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Danietha Tindamanyere akizungumzia mpango wa mabadiliko ya Sekta ya Mifugo na maboresho ya Sera ya Mifugo wakati wa siku ya kwanza ya mafunzo rejea kwa baadhi ya maafisa ugani (hawapo pichani) kutoka Kanda ya Ziwa Mashariki inayohusisha mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera. Mafunzo haya ya siku mbili yanafanyika katika Mji wa Maswa, Mkoani Simiyu. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Na. Edward Kondela
MAAFISA ugani kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa Mashariki wametakiwa kuhakikisha wanawasaidia wafugaji kufuga kibiashara na kuachana na ufugaji usio na tija.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Mhe. Aswege Kaminyonge amebainisha hayo leo (12.12.2022) Mjini Maswa, wakati akifungua rasmi mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa ugani kutoka mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera na kuwataka maafisa hao kuwasaidia wafugaji kwa kuwapatia elimu ya ufugaji na kuipatia mifugo yao chanjo ili kufuga kwa tija.

Mhe. Kaminyonge ameongeza kuwa endapo wafugaji wakielimishwa na kuhamasishwa hawana shida katika kufanya mabadiliko kwenye ufugaji bora na kibiashara kwa kuzingatia pia uogeshaji wa mifugo na kilimo cha malisho ya mifugo katika maeneo yao.

“Naona jinsi ilivyo rahisi kutoa elimu kwa wafugaji hususan kwa wafugaji ambao wanafuga kiholela bila kuzingatia matumizi bora ya ardhi, inatakiwa kila mfugaji kuwa na eneo la kufuga na kuligawa kwa malisho na mifugo yake.” Amesema Mhe. Kaminyonge

Aidha, amesema mifugo mingi imekuwa ikila mchanga badala ya malisho bora ambayo yanaweza kuleta tija kwa kutoa mazao bora yanayotokana na mifugo hiyo kama maziwa na nyama na kukosa ubora unaotakiwa.

Akizungumza kando ya kikao hicho Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Ugani) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samwel Mdachi amesema mafunzo hayo yanafanyika katika kanda tano nchini ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za wizara kuwaongezea uwezo maafisa ugani ili kuwasaidia wafugaji katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Bw. Mdachi amesema mafunzo hayo ambayo yanafanyika kwa awamu ya pili sasa ikiwa ni moja ya mikakati ya kuleta mabadiliko katika Sekta ya Mifugo nchini ambapo eneo linalowekewa mkazo ni kuimarisha huduma za ugani ambapo wizara kwa mwaka huu wa fedha imepanga kuwafikia maafisa ugani 800 kote nchini.

Nao baadhi ya maafisa ugani wanaoshiriki mafunzo hayo wamesema, ni wakati sasa kwa wao kuwasaidia zaidi wafugaji namna ya kufuga kibiashara pia namna ya kutokomeza magonjwa ya mifugo ambayo yamekuwa yakiathiri shughuli zao.

Wamebainisha kuwa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi yatakuwa na tija kwao kwa kuwa watajifunza mambo mengi kulingana na mabadiliko ya tabia ya nchi hali ambayo pia inaweza kuwasaidia wafugaji.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...