Prof. Shani Omari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (anayezungumza, wa kwanza kulia) akitoa hoja kwenye mdahalo ulioandaliwa kwenye Kongamano la Kumuenzi Hayati Bibi Titi Mohammed, wa pili ni Nguli wa Lugha ya Kiswahili, Prof. Aldin Mutembei, wa tatu ni Bi. Kate Kamba.
Nguli wa Kiswahili, Prof. Aldin Mutembei akizungumza kwenye Kongamano hilo.



Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
NI takribani miaka 22 sasa tangu kufariki dunia kwa Bibi Titi Mohammed ambaye alikuwa Mwanamke shupavu na jasiri katika harakati za kudai uhuru wa taifa la Tanzania akisaidiana na Waasisi wengine, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wengine wengi.

Hayati Bibi Titi Mohammed hakubahatika kupata elimu kubwa, kama walivyobahatika Viongozi wengine wa masuala ya Siasa, lakini Titi Mohammed alikuwa na kipaji cha hali ya juu, alijaaliwa kuwa Muhamasishaji mahiri wa harakati za kudai uhuru hususani kwa Wanawake ambao hawakupewa kipaumbele zaidi kipindi cha enzi za Mkoloni.

Mtaalamu wa Lugha ya Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Aldin Mutembei amemzungumzia Hayati Bibi Titi kuwa ni Mwanamke ambaye ameifundisha jamii mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuwa jasiri na uthubutu wa kuhimiza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.

“Tunakumbuka miaka ya 1960, alihamasisha Bunge la Tanzania kuzungumza lugha ya Kiswahili, na hadi leo tunazungumza lugha hiyo baada ya Kiongozi wa juu wakati huo, Mwalimu Nyerere kuona umuhimu wa matumizi ya lugha hiyo bungeni”, amesema Prof. Mutembei.

“Hayati Mwalimu Nyerere alimtumia sana Bibi Titi katika mikutano yake, ilikuwa kabla ya kuanza kuhutubia Wananchi, aliitwa Bibi Titi kuimba nyimbo mbalimbali za lugha adhimu ya Kiswahili zenye ulumbi ndani yake ili kuhamasisha Wananchi hao kusikiliza kwa makini mkutano mikutano mbalimbali”, ameeleza Prof. Mutembei kwenye kongamano maalum la Kumbukizi ya Hayati Bibi Titi, Rufiji mkoani Pwani.

Kwa upande wake, Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Kate Kamba amesema alifanikiwa kumuona na kumshuhudia Bibi Titi ambaye alikuwa na maono makubwa katika kumkomboa Mwanamke na harakati za kulikomboa taifa la Tanzania kutoka mikononi mwa Wakoloni.

Bi. Kate Kamba amesema Hayati Bibi Titi alishiriki kikamilifu katika kuanzishwa kwa Umoja wa Wanawake Tanzania na Umoja wa Wazazi, pia alifanya kazi sanjari na kusafiri hadi nchi jirani ya Kenya katika kusaidia harakati za ukombozi wa taifa hilo kutoka kwa Mkoloni.

“Wazungu hawakutaka Waafrika tupate elimu, hawakuta sisi tupate elimu kubwa, lakini Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wapigania uhuru wengine wakina Bibi Titi walihakikisha taifa linakombolewa na kuondokana na hali hiyo ukoloni”, amesema Bi. Kate Kamba.

Naye, Prof. Shani Omari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye alimwakilisha Waziri wa Elimu, amesema Bibi Titi alikuwa mtumia na mchukua fursa kwa kuona mapema fursa za harakati za ukombozi akiwa Mwanamke, na alisimama kidete katika masuala ya Siasa na kutoa hamasa kwa wenzake kudai uhuru kutoka kwa Mkoloni.

Prof. Shani amesema Chama cha TANU kilimpa nafasi Bibi Titi katika ulingo wa Siasa baada ya kuona mumewe kuwa Mwanachama wa Chama hicho na yeye aliamua kumuunga mkono kwa vitendo harakati hizo, ikiwemo kuhamasisha Wanawake wenzake kuungana katika harakati za kujikomboa kisiasa.

“Alitumia fursa na alianza kumfuata mumewe akiwa na Kadi ya Uachama namba 15 na yeye Bibi Titi alikuwa na Kadi ya Uanachama namba 16, wote walifanya Siasa ijapokuwa baadae aliachwa na mumewe kwa sababu ya kufanya harakati hizo za kutaka kumkomboa Mwanamke, huu ulikuwa msimamo wake”, amesema Prof. Shani.

Prof. Shani amesema: “Elimu ndogo aliyokuwa nayo Hayati Bibi Titi, haikuzuia kufanya harakati za Siasa na aliweza kuchukua kila kitu, hasi au chanya katika kuhakikisha anafanikiwa kuimarika katika masuala hayo ya Siasa na wala hakukata tamaa”.

Hayati Bibi Titi Mohammed alizawali mwaka 1926, Temeke na alifariki mwaka 2000. Enzi za uhai wake alikuwa Mwanaharakati wa ukombozi wa uhuru wa taifa la Tanzania akisaidiana na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...