SERIKALI ya Tanzania imeikabidhi Burundi kiti cha uenyekiti wa Mawaziri waliopo katika Mkataba wa Kikanda wa Usimamizi Endelevu wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika na kusisitiza Kiswahili kitumike kama lugha kuu ya mawasiliano katika mikutano yote itakayofanyika.
Hayo yamejiri wakati wa Mkutano wa 10 wa Mawaziri hao uliofanyika jana jijini Bujumbura nchini Burundi baada ya Tanzania kumaliza muda wa uenyekiti uliodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo kwa Waziri wa Mazingira, Kilimo na Mifugo wa Burundi Prof. Sanctus Niragira, amesema Tanzania inashiriki katika shughuli zote zinazolenga kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za ziwa hilo.
Pia, amesema Tanzania imedhamiria kushirikiana na nchi wanachama ambazo ni Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Jamhuri ya Zambia katika utekelezaji wa programu za kikanda zinazolenga kulinda rasilimali za pamoja za Ziwa Tanganyika na kuboresha maisha ya watu katika ukanda huo.
Dkt. Jafo amesema Ziwa Tanganyika ni rasilimali muhimu kwa wananchi takriban milioni 10 wa ukanda huo wanaolizunguka hivyo zinahitajika juhudi za pamoja katika kulilinda.
“Waheshimiwa mawaziri, mazingira tunayoishi yanabadilika haraka sana na shughuli za binadamu zinatumia maliasili za dunia kwa kasi ya kutisha na kuharibu mifumo ikolojia.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya viumbe 22,000 wako hatarini kutoweka ikiwa ni pamoja na baadhi ya viumbe katika Ziwa Tanganyika,” amesema.
Hivyo, ametoa wito kwa Mawaziri hao kutoka nchi wanachama kuungana kwa pamoja kujadili namna bora ya kulinda Ziwa Tanganyika kwa manufaa ya kizazi cha leo na kizazi kijacho huku akisisitiza umuhimu wa kuweka utaratibu wa muda mrefu wa ufadhili wa programu ya maendeleo ya Ukanda ya Ziwa Tanganyika.
Aidha Mkutano huo wa nchi wanachama wa Mkataba wa hifadhi na Usimamizi endelevu wa Ziwa Tanganyika ulifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Prosper Bazombanza.
Ujumbe ulioshiriki katika Mkutano huo uliwashirikisha pia Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama, Mkurugenzi wa Mazingira Dkt. Andrew Komba, Afisa Mazingira Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Deogratius Nyangu na uwakilishi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja ba Wizara ya Uvuvi na Mifugo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...