KATIBU mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania – TFF Wilfred Kidau ameeleza
kufurahishwa kwake na kazi inayofanywa na shirika lisilo la kiserikali
la Karibu Tanzania Organization (KTO) katika kuendeleza soka la wanawake
nchini.
Kidau amesema hayo wakati akifunga mafunzo
ya uongozi katika michezo kwa makocha wanawake 42 kutoka Vyuo vya
Maendeleo ya Wananchi, kupitia Programu ya Mpira Fursa inayoendeshwa na
KTO. Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika jijini Dar es salaam,
yameendeshwa na wataalamu kutoka Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
Amesema
ili kuunga mkono jitihada hizo, mapema mwaka 2023 TFF itaendesha kwa
gharama zake mafunzo ya aina tatu ya soka kwa wanawake hao ikiwemo
ukocha/ualimu, uamuzi (referee), na usimamizi/uongozi. Pia ametoa zawadi
ya mipira miwili kwa kila mshiriki wa mafunzo hayo baada kuwapongeza
kutokana na nidhamu waliyoionyesha katika kipindi chote cha mafunzo.
Kwa
upande wake mwakilishi wa kurugenzi ya elimu na mafunzo ya ufundi
(TVET) katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi Fides Lubuva,
amepongeza ushirikiano ulioonyeshwa na TFF katika kuendeleza programu
hii ambayo ilianzishwa kwa ushirikiano baina ya KTO na TFF. Amewataka
makocha hao kuhakikisha FDCs inakuwa na timu imara ili ziweze kushiriki
michuano hadi ngazi ya taifa na kutoa wachezaji bora watakaoliwakilisha
taifa katika michuano mikubwa.
Programu ya Mpira
Fursa inalenga kukuza na kuendeleza soka la wanawake na wasichana kwa
kuandaa wanasoka bora wa kike wenye kujiamini na kujithamini, na kama
njia ya kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi.
Programu hii inatekelezwa katika vyuo 54 vya mMaendeleo ya Wananchi kwa
ufadhili wa Sida na MasterCard Foundation; na katika shule 108 za msingi
kwa ufadhili wa taasisi ya Watoto ya shirikisho la soka barani Ulaya
UEFA Foundation.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...